Chuo cha Ufundi Stadi
cha Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga kimeanza kutoa bure huduma ya ufundi umeme
wa majumbani (wiring) kwa kaya 50 zenye kipato cha chini katika Tarafa mbili
wilayani humo.
Akizungumza jana tarehe 21 Novemba, 2024, wilayani Mkinga wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, amepongeza mpango huo na kusema kuwa chuo hicho kimeonesha umuhimu wake kwa jamii ya Mkinga.
Amesema ubunifu huo ni
sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuonesha tija waliyoipata vijana wanaosoma
chuoni hapo.
Sambamba na hilo, Kalima amesema chuo hicho pia kimesaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha mafundi wenye ujuzi, wengi wao wakiwa kutoka wilaya ya Mkinga, hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mafundi umeme wilayani humo.
“Kwa muda mrefu,
mafundi umeme wengi waliokuwa wakifanya kazi wilayani Mkinga walikuwa wakitoka
Tanga mjini na baadhi yao kutoka nje ya mkoa wa Tanga, na tatizo kubwa lilikuwa
ni kukosa uaminifu na baadhi yao kudhulumu wananchi. Lakini sasa, kupitia chuo
cha VETA, tunapata mafundi waliopata mafunzo bora na wanaoweza kutoa huduma kwa
ufanisi,” amesema Mhe. Kalima.
Ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanapeleka vijana wao katika chuo hicho ili waweze kupata ujuzi mbalimbali kupitia kozi zinazotolewa, ambazo ni za muda mrefu na mfupi.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Chuo cha VETA Wilaya ya Mkinga, Calvin Haule, amesema kuwa mpango huo
unalenga kusogeza huduma ya umeme kwa jamii na kupunguza gharama ya kulipa
mafundi kutoka maeneo ya mbali.
Haule ameongeza kuwa
mpango huo pia utawawezesha wanafunzi kujiimarisha kwenye mafunzo kwa vitendo
na kwamba huduma hiyo itasaidia kaya kuboresha maisha yao na kukuza shughuli za
kiuchumi zinazotokana na nishati ya umeme.
No comments:
Post a Comment