Mkurugenzi wa Kanda ya
Mashariki, John Mwanja ameelekeza vyuo vya VETA Kanda ya Mashariki kutoa
mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo kuwasaidia vijana kujiajiri baada ya
kuhitimu mafunzo yao.
John Mwanja, ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 36 ya wanafunzi wa ngazi ya II katika chuo cha VETA Kihonda, yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho, tarehe 21 Novemba 2024.
Amewataka walimu na menejimenti za vyuo vya VETA kuwasaidia na kuwasimamia wanafunzi kuanzisha vikundi, kupanga na kutekeleza mawazo ya kuanzisha makampuni madogo madogo wakiwa darasani, ili kuwazoesha kuungana na kufanya kazi kwa pamoja, kujiajiri na kutafuta soko la bidhaa zao.
“Hivyo, ni jukumu la menejimenti kuwasaidia wanafunzi waliojiunga kwenye vikundi vidogo vidogo kwa fani mbalimbali, kurasimisha vikundi hivyo ili bidhaa zitakazozalishwa ziweze kuingia sokoni,” Mwanja amesema
Mkurugenzi huyo,
amesisitiza menejimenti kutoa mafunzo ya ujuzi yenye tija yanayolenga kuzalisha
bidhaa zenye ubora kukidhi ushindani na kutafuta soko ili kupata marejesho ya
bidhaa hizo kupitia fedha za mauzo.
Aidha, Mwanja ametaka bidhaa zinazotengenezwa na wanafunzi wakati wa mazoezi ya vitendo zitafutiwe soko na kama inashindikana kupata soko zitolewe kwa watu wenye mahitaji maalum badala ya kurundikana katika karakana.
Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda, Dkt. Salumu Ulimwengu, amewapongeza wahitimu na kuwataka Kwenda kutumia ujuzi katika kuwaendeshea maisha yao na kuwa mfano wa kuigwa na jamii itakayowazunguka.
“Nendeni mkawe mabalozi
wazuri, mkatumie elimu ya ufundi stadi mliyoipata kuwaletea kipato,”
Dkt.Ulimwengu amesema.
Mahafali hayo
yalijumuisha wahitimu 230 wa ngazi ya II wakiwemo wakike 62 na wakiume 168
katika fani za Zana za Kilimo (wahitimu 25), Umeme wa magari (23), umeme majumbani
(42), Bomba (37), Useremala (11), Uashi (21), Majokofu na Viyoyozi (32),
Ushonaji (16), Ufundi magari (21), na Mitambo na Ukerezaji (16). Pia wanafunzi
132 wa udereva na kozi za muda mfupi wamehitimu.
No comments:
Post a Comment