Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore ameagiza
uongozi wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kutangaza zaidi
kozi zinazotolewa na chuo hicho ili kuongeza udahili.
CPA Kasore ametoa
maagizo hayo tarehe 5 Desemba, 2024 alipotembelea na kukagua hali ya utoaji
mafunzo katika chuo hicho.
Kasore amesema kwa
sasa kuna ongezeko kubwa la uhitaji wa walimu wa kufundisha vyuo vya Ufundi
Stadi hapa nchini kutokana na Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika ujenzi vyuo
vya ufundi stadi.
"Kwa sasa tuna
vyuo vya VETA kila Mkoa na tunajenga vyuo katika kila wilaya… vyuo hivi vyote
vitahitaji walimu wa kufundisha na chuo hiki cha MVTTC ndio chuo kinachoandaa
walimu wa ufundi stadi hapa nchini," amesema CPA Kasore.
Kasore amesema kuwa
chuo hicho kina programu nyingi na nyingine zinatolewa kwa masafa yaani
"outreach programme", hivyo zinapaswa kutangazwa ili wananchi waweze
kuzifahamu na kuzitumia.
Sambamba na hilo CPA
Kasore amewahimiza MVTTC kutunza vifaa vya kufundishia vilivyopo katika chuo
hicho na kuvitumia vyema katika mafunzo na uzalishaji.
Kwa upande wake Mkuu
wa chuo hicho, Samweli Kaali amesema menejimenti ya MVTTC itafanyia kazi kwa
makini maelekezo yote yaliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu ili kuimarisha ufanisi wa
utoaji mafunzo chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment