Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepokea tuzo ya heshima kwa mchango wake wa
kipekee katika kutatua changamoto za kijamii kupitia sayansi, teknolojia, na
ubunifu.
Tuzo hiyo imetolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na kukabidhiwa na Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, aliyekuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya kuhitimisha Kongamano na Maonesho ya 9 ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE), leo tarehe 4 Desemba, 2024, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kutambua historia na maonesho ya ubunifu mbalimbali, ubunifu mahsusi wa VETA uliotambuliwa katika STICE 2024 ni Dawa Asili ya Mafuta ya Kuua Mbu (Natural Jelly Oil Mosquito Repellant), iliyobuniwa na mwalimu Ally Issa kutoka Chuo cha VETA Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya
kupokea tuzo hiyo, Mwalimu Issa alisema wazo la kubuni dawa hiyo lilichochewa
na changamoto ya mbu inayowakumba watu wengi nchini, hususan kabla ya kulala.
“Dawa nyingi za kuua mbu zina kemikali zinazoweza kusababisha mzio wa ngozi. Hii ilinifanya nifikirie suluhisho mbadala kwa kutumia mimea na matunda ambayo hayana madhara. Hata kama dawa itaingia kinywani kwa bahati mbaya, haina athari kwa mwili. Msemo ninaotumia sana ni kuwa, ‘Kisicholika usikitumie kupaka,’” amesema Issa.
Ubunifu wa dawa hiyo, ambao umekamilika mwaka huu, umeonyesha uwezo wa matumizi ya malighafi za asili kutatua changamoto za kiafya huku ukizingatia usalama wa watumiaji.
Tuzo hii ni ushuhuda
wa dhamira ya VETA ya kuendeleza vipaji na bunifu zinazoweza kubadili maisha ya
Watanzania kwa kutumia elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Sambamba na tuzo hiyo, VETA pia imekabidhiwa ngao kutambua mchango wake katika kuwezesha STICE 2024.
STICE 2024 imefanyika
kuanzia kuanzia tarehe 2 hadi 4 Desemba 2024.
No comments:
Post a Comment