Jumla ya Maafisa
Ununuzi na Ugavi 120 kutoka Kanda zote za Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA) wanashiriki katika mafunzo elekezi jijini Dodoma kwa lengo la
kuwajengea uwezo, hivyo kuimarisha utendaji kazi wao.
Akizungumza leo tarehe 9 Machi, 2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi, VETA, Bi. Witness Mgimba amesema mafunzo hayo elekezi yameanza kutolewa tarehe 5 Machi, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha VETA Dodoma kwa kushirikiana na Maafisa Ununuzi wa VETA Makao Makuu, wataalam kutoka PPRA na wataalam kutoka Hazina, na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 12 Machi, 2026
“mafunzo haya
yanalenga kuimarisha utendaji kazi, kuhakikisha ufanisi, utunzaji wa mali za
umma, matumizi ya mfumo wa Uhasibu Seriakalini (MUSE), kushirikisha makundi
maalum katika ununuzi wa umma na kufuata taratibu za Serikali katika
utekelezaji wa majukumu ya kila siku,” amesema Bi Mgimba.
Sambamba na kupatiwa mafunzo hayo Bi Mgimba amesema watumishi hao watawasilisha changomoto wanazokutana nazo katika utendaji kazi wao wa kila siku ili kwa umoja wao waze kuzipatia ufumbuzi.
Hata hivyo Bi mgimba
amesema watumishi hao wanaendelea kupewa maelekezo katika eneo la usimamizi wa
ugavi kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Sheria ya Ununuzi wa Umma ya
mwaka 2020/2023 ambayo inasisitiza utunzaji wa vifaa,vitendea kazi
vinavyonunuliwa ili kutoisababishia Serikali hasara kwa kutokutunza vifaa hivyo
au kuvifanyia matumizi yasiyokuwa sahihi.
Aidha Bi Mgimba ameishukuru Menejimenti ya VETA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu kwa kutoa kibali kwa maafisa hao kushiriki katika mafunzo hayo.
Kwa upande wake Jacqline Sebastian, Afisa Ununuzi Mwandazi kutoka MVTTC amesema amejifunza mambo mengi katika ununuzi wa umma ikiwa ni pamoja na kuhusisha Makundi Maalum kwenye ununuzi wa umma, ambapo makundi hayo yanajumuisha wanawake,vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
Paul Mshabaha, Afisa
Ununuzi kutoka Chuo cha VETA Iringa na mnufaika wa mafunzo hayo amesema,
“Naishukuru VETA kwa kuandaa mafunzo haya hasa kwetu sisi ajira mpya,
nimejifunza utunzaji wa mali za serikali,mfumo wa ulipaji Serikalini (MUSE),
lakini tunatarajia kujifunza maadili ya utumishi umma ili tuweze kwenda
kuwajibika kwa kufuata miongozo na taratibu za kiutumishi.”
VETA imekuwa ikitoa
mafunzo elekezi kwa watumishi wa kada ya ununuzi na ugavi ili kuelewa majukumu na kuwajenga uwezo ili
kufikia malengo ya Serikali na kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi.




No comments:
Post a Comment