CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Saturday, 7 March 2026

Zaidi ya Vijana 5,600 Kunufaika na Mradi wa YEFFA

               

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema matumizi sahihi ya teknolojia katika kilimo yanaweza kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, hatua itakayosaidia kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Amesema hayo tarehe 5 Machi , 2026 wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Ujasiriamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (YEFFA) uliofanyika katika Chuo cha VETA Kihonda mkoani Morogoro.

Amesema mradi huo unalenga kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo katika ufundi wa zana za kilimo, teknolojia za umwagiliaji na uhifadhi wa mazao baada ya mavuno ili kukabiliana na changamoto za uzalishaji na upotevu wa mazao.

“Mmepata wazo zuri la kubuni mradi utakaosaidia kujibu changamoto ya mahitaji ya ujuzi katika ufundi wa zana za kilimo, teknolojia ya umwagiliaji na uhifadhi wa mazao pamoja na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno,” amesema Ameir.

Ameongeza kuwa uzinduzi wa mradi huo ni hatua muhimu katika kuwawezesha vijana wa Tanzania kupata ujuzi, ajira na fursa za ujasiriamali, hususan katika sekta ya kilimo ambayo ni mhimili wa uchumi wa Taifa.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mkazo katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa na yenye tija zaidi.

“Sekta ya kilimo inaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwa kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la Taifa,” amesema.

Kwa mujibu wa waandaaji, zaidi ya vijana 5,631 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo ambao unatekelezwa chini ya uratibu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mpango wa Kilimo cha Vijijini na Mijini

(RUATI),

Wengine ni Taasisi ya Ujasiriamali wa Vijijini (AMSHA), Chama cha Uendelezaji wa Matumizi ya Mitambo ya Kilimo Tanzania (TAMA) na Shirika la Kuboresha na Kuimarisha Huduma za Mashirika (MIBOS).

Mafunzo hayo yatatolewa katika vyuo vinne vya VETA ambavyo ni VETA Kihonda, VETA Manyara, VETA Mpanda na VETA Arusha.

Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili ukiwa na awamu 11 za udahili na unatarajiwa kuwafikia vijana kutoka mikoa 19 nchini, wakiwemo vijana wa vijijini na mijini kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, amesema mradi wa YEFFA una thamani ya dola za Marekani milioni 1.4, sawa na takribani Sh. za Tanzania Bilioni 3.5, fedha zinazotokana na ufadhili wa taasisi ya Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA).

Kasore amesema zaidi vijana 700 wamedahiliwa na kuanza mafunzo katika stadi mbalimbali chini ya mradi huo.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi stadi, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mafunzo, pamoja na kutoa fursa zaidi za ajira na mafunzo kwa vitendo kwa vijana.

Amesema hatua hizo zitahakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na ajenda ya kilimo cha kisasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) Tanzania, Vianney Rweyendela, amewataka vijana waliopata mafunzo kupitia mradi huo kuwafundisha wenzao katika jamii ili kuongeza idadi ya vijana wenye ujuzi katika sekta ya kilimo.

Pia ameitaka serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika kuwajengea vijana uwezo katika kilimo-biashara, maendeleo ya ujuzi na ubunifu.

Naye mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Abra Kingologo, ambaye pia ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, amesema aliamua kujiunga na mafunzo hayo ili kuongeza ujuzi katika matumizi ya mitambo ya kilimo.

“Mimi kama msichana sikuona aibu pale serikali ilipotangaza fursa hii. Nikaona ni vyema kujifunza kwa manufaa yangu, taifa na jamii niliyotoka, ingawa baadhi ya wasichana wanaona kama ni ajabu,” amesema.

Ameongeza kuwa ujuzi alioupata utamwezesha kufanya kilimo cha kisasa na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo katika eneo analotoka

No comments:

Post a Comment