WAJASIRIAMALI zaidi ya 200 katika Kata
ya Bunju jijini Dar es Salaam wamepata mafunzo ya siku 10 katika ujuzi mbalimbali
ili kuwasaidia kukuza ujasiriamali na kuongeza kipato katika familia na jamii
kwa ujumla.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Kanda ya Dar es Salaam kuanzia tarehe
14 hadi 25, November 2016 chini ya Mpango wa Kukuza Ujasiriamali katika Sekta
isiyo Rasmi (INTEP) na yalihusisha stadi za utegenezaji wa Batiki, Mapishi, Mapambo na Ufundi wa Upakaji rangi.
Akizungumza
katika hafla ya kufunga Mafunzo hayo siku ya Ijumaa November 25, 2016 Afisa
Mtendaji wa Kata ya Bunju Shumasike Shumasike alisema, mafunzo hayo yameongeza
fursa ya ajira kwa wananchi wake na kuiomba VETA kuendelea kutoa mafunzo ya
namna hiyo zaidi kwani yatawasaidia wananchi wa kawaida kwa kiasi kikubwa.
Alisema, waliopata mafunzo ni watu
ambao walikuwa hawana shughuli yeyote ya kuwaingizia kipato hivyo kupata
mafunzo yameonyesha njia ya kuweza kuingia katika soko la ajira kwa kuanzisha
biashara mbalimbali.
Shumasike aliwaasa wanufaika wa mafunzo
kutumia vyema vyeti walivyovipata na kuidhihirishia jamii kuwa ujuzi walioupata
ni wa manufaa makubwa kwao na kwa jamii inayowazunguka na sio kurudi katika
hali waliyokuwa nayo mwanzo.
Alisema fedha ya ahadi ya Rais
iliyotolewa kwa kila mtaa kunufaika na sh. Milioni 50 kwa ajili ya wajasirimali
zitatolewa kwa vikundi na sio kwa mtu mmoja mmoja hivyo wajiandae kwa
kutengeneza vikundi na kuvisajili ili fedha hizo zitakapowasili waweze
kunufaika.
Naye Mkurugenzi wa Kanda ya VETA Dar es
Salaam, Habib Bukko alisema anaamini waliopata mafunzo hayo watayatumia
ipasavyo katika kubadilisha maisha yao na kwamba VETA inaendelea na juhudi za
kuhakikisha mafunzo hayo yanafikia makundi mengi zaidi.
Mmoja ya walionufaika na Mafunzo hayo, Joyce Lweganwa amesema watatumia mafunzo hayo katika kutengeneza kipato na kuitaka VETA kufikia watu wengine kutokana na ukweli kwamba wahitaji wa mafunzo ya aina hiyo ni wengi sana katika jamii.
No comments:
Post a Comment