Mamlaka
ya Elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na kampuni ya simu
za mkononi Airtel kupitia programu ya utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa
njia ya simu (VSOMO) wamezindua namba maalum kwa ajili ya kuwahudumia wananchi
kwa karibu zaidi.
Mgeni
rasmi katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Habibu
Bukko amesema kupitia namba 0699859573 na 0699859572 wananchi watapata
maelekezo yote muhimu yanayohusiana na VSOMO.
Amesema
lengo la VETA ni kuendelea kuwawezesha watanzania kushiriki kikamilifu katika
sera ya uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha wanapata ujuzi popote pale
wanapokuwa.
“Wananchi
wanaweza kupiga simu namba 0699859573 na 0699859572 kila siku kuanzia saa 2
asubuhi hadi saa 10 jioni na kuuliza maswali, ufafanuzi na kutoa mapendekezo
juu ya programu ya VSOMO na kupata majibu papo kwa hapo”Alisema
Mkuu
wa Chuo cha VETA Kipawa ambaye pia ni mratibu wa VSOMO Eng. Lucius Luteganya
amesema mwitikio wa wananchi na hasa vijana katika programu hiyo ni wa kuridhisha
na kwamba takwimu zinaonyesha zaidi ya vijana 30,000 tayari wamepakua
application ya VSOMO, 8000 wamejiandikisha na kati yao 50 wanasoma kozi
mbalimbali na wengine tayari wameshahitimu na kupata vyeti vya VETA.
“Tumeona
kuna umuhimu wa kuweka namba hizi maalum ili kuweza kuwahudumia wananchi kwa
karibu zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho mpango huu wa VSOMO unazidi
kupanuka kwa kuongeza kozi nyingi kulingana na mahitaji” Alisema
Alizitaja
kozi zinazopatikana kwa njia ya VSOMO kwa sasa ni Huduma ya chakula na mbinu za
kuhudumia wateja, Matengenezo ya Kompyuta, Umeme wa viwandani, Ufundi Bomba wa
Majumbani, Umeme wa magari, Ufundi umeme
wa majumbani, Ufundi pikipiki, Ufundi wa simu za mkononi, Ufundi Alluminium,
Utaalamu wa maswala ya urembo pamoja na Ufundi wa kuchomea vyuma.
Meneja
Uhusiano wa Airtel Jackson Mbando alisema kampuni yake inajisikia fahari
kuendelea kuongeza ubunifu katika programu ya VSOMO na lengo ni kuboresha na
kurahisisha upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Alisema
kila simu itakayopigwa itachajiwa gharama ya shilingi 60 tu na kwamba mteja
hatapangiwa muda wa kuongea na mtoa huduma hadi mwisho wa kuhudumiwa.
Programu
ya utoaji wa mafunzo kwa njia ya simu (VSOMO) ilizinduliwa mwezi June 2016
ambapo wananchi wanaweza kupakua application hiyo kutoka kwenye Google Play
Store na kujisajili na kuanza masomo kwa njia simu na wakifaulu huchagua chuo
wanachopenda kuhudhuria mafunzo ya vitendo na wakifaulu hutunukiwa vyeti vya
VETA.
No comments:
Post a Comment