Kwa mara nyingine tena Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepata ushindi wa kwanza kwenye kundi la Taasisi za Utafiti na Mafunzo katika maonesho ya Wakulima Nanenane, 2017 yaliyokuwa yakifanyika kitaifa kwenye uwanja wa Ngongo mkoani Lindi.
VETA ilifuatiwa na Chuo cha Maji katika nafasi ya pili na Chuo cha Uhasibu Arusha ambacho kilishika nafasi ya tatu katika kundi hilo.
Kaulimbiu
ya maonesho hayo ilikuwa, "Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo,
Ufugaji na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati."
Vilevile
VETA ilionesha ubunifu wa teknolojia bora na rahisi katika kilimo, mifugo na
uvuvi na kwa ajili ya kuboresha maisha ya jamii ya wananchi wa kijijini.
Katika maonesho hayo VETA imepokea wageni mbalimbali ikiwemo viongozi wa kitaifa ambao kwa pamoja walikiri kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na vyuo vya ufundi stadi nchini hasa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini huku wakishauri kutanua wigo wa utoaji mafunzo ili kufikia makundi mengi zaidi.
Mkuu
wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliiomba VETA kushirikiana na jeshi hilo
kuandaa mafunzo maalum ya ufundi stadi kwa vijana wanaojiunga na kambi za JKT
katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo la ombi hilo ni kuhakikisha kuwa vijana
hao wakimaliza mafunzo ya jeshi watoke pia na ujuzi na vyeti vinavyotambulika
na VETA na kukubalika kitaifa.
Akizungumzia ushindi huo, Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter alisema, ni ishara kuwa jamii na mamlaka mbalimbali wanazidi kutambua na kuamini mchango muhimu unaotolewa na VETA.
Aliwaasa wakulima na wanajamii kuendelea kutumia fursa mbalimbali za mafunzo zinazotolewa na VETA ili waweze kunufaika kwa kupata ujuzi utakaoweza kuwasaidia kuongeza tija katika uzalishaji na kujipatia ajira na kuongeza vipato vyao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment