Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetiliana saini makubaliano yenye
thamani ya Euro 900,000 (zaidi ya shilingi bilioni 2.3) na Chemba ya Baraza la
Ufundi Stadi ya Ujerumani (WHKT) kwa ajili ya mafunzo ya uwanagenzi yenye lengo
la kuimarisha ufundi wa zana za kilimo na teknolojia ya mitambo ya ujenzi.
Makubaliano
hayo yalitiwa saini Alhamisi, 17 Agosti, 2017 na Moshi Kabengwe, Mkurugenzi wa
Utawana na Usimamizi wa Rasilimali watu, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo kwa upande wa Tanzania na
Mtendaji Mkuu wa WHKT, Bw. Reiner Nolte kwa upande wa Ujerumani.
Utiaji
saini makubaliano hayo ulishuhudiwa na Barozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter, Mwenyekiti wa Board ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Bw. Peter
Maduki, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Dk. Bwire Ndazi na Maafisa wengine waandamizi
wengine wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, VETA na Ujerumani.
Waraka wa
makubaliano hayo unaeleza kuwa utekelezaji wa mradi utaanza mara baada ya
kusaini hadi tarehe 31 Machi, 2020, lakini kuna fursa ya kuongeza muda zaidi
kutegemeana na uzoefu kutoka katika mradi wa awali na makubaliano ya pande zote
mbili.
“ujuzi wa mafundi na wakulima utaboreshwa kupitia kozi zitakazotolewa
na VETA kwa mfumo wa uwanagenzi. Kozi hizo ni pamoja ufundi zana za kilimo,
ufundi mitambo ya ujenzi na mafunzo ya vitendo katika teknolojia ya kupunguza
upotevu wa mavuno ya mazao ya kilimo katika maeneo yatakayoainishwa,” inaeleza
sehemu ya waraka wa makubaliano.
Utekelezaji wa
mradi huo unakuja baada ya kupata uzoefu wa ushirikiano katika mradi
mwingine kati ya VETA na Chemba ya Ufundi Stadi ya Ujerumani kwenye mafunzo kwa
njia ya uwanagenzi katika fani za ufundi magari, ufundi umeme na huduma za
hoteli ambao umekuwa ukitekelezwa tangu mwaka 2011 hadi sasa. Uwanagenzi ni
mfumo unaohusisha mafunzo yanayohusisha ngwe za mzunguko kati ya chuo cha
ufundi na sehemu ya kazi.
Akizungumza
wakati wa kusaini makubaliano hayo, Balozi wa Ujerumani nchini Dk. Detlef Waechter alisema anatarajia kuwa ushirikiano katika mradi huo utawasaidia kwa
kiasi kikubwa Watanzania wengi, hususani vijana katika kupata ujuzi wa kuutumia
katika kuongeza tija kwenye kilimo nchini.
Alisema,
Ujerumani ina uzoefu mkubwa na wa muda mrefu katika utoaji mafunzo kwa njia ya uwanagenzi na kwa hivyo Tanzania
ina mengi ya kujifunza kutoka Ujerumani.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimani watu kutoka Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknoloji Bw. Moshi Kabengwe aliishukuru serikali ya
Ujerumani kwa msaada na ushirikiano na kusema kuwa utawasaidia vijana wengi
kuajirika na kuwa na ujuzi wa kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo.
Naye Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire Ndazi aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa
kuendelea kuiamini VETA na kuendeleza ushirikiano nayo katika utoaji mafunzo kwa
mfumo wa uwanagenzi.
Alisema,
ushirikiano katika miradi ya nyuma umeendelea kuwanufaisha vijana wengi kupata
ujuzi na kuweza kuajirika kwa urahisi.
Mafunzo ya
uwanagenzi huendeshwa kwa mfumo wa ngwe za mzunguko kati ya chuo cha ufundi
stadi na sehemu ya kazi ambapo
mwanafunzi hupata mafunzo ya ujuzi kwenye karakana za chuo na uzoefu wa
hali halisi mahala pa kazi, hivyo kumwongezea umahiri pamoja na maarifa zaidi
na utamaduni wa ya mazingira ya kazi husika.
No comments:
Post a Comment