CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Thursday, 31 August 2017

VETA kurasimisha ujuzi wa vijana 3,900 nchini



Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)  chini ya ufadhili wa ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi ,Vijana, Ajira Wenye Ulemavu  imezindua awamu ya tatu ya  zoezi la kurasimisha ujuzi wa mafundi wasiopungua 3,900 nchini.

Akizungumza wakati wa  uzunduzi wa  zoezi hilo katika mikoa ya Morogoro, Dar es salaam, Pwani, Lindi na Mtwara,   Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi ,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu  Mh. Anthony Mavunde kutumia vyema fursa hiyo kwani itawawezesha kuboresha kazi zao na kuzifanya zikubalike kwenye mfumo rasmi.

Alisema kupitia zoezi hilo mafundi waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi watafanyiwa tathmini  kulingana na ujuzi walionao kisha kupewa mafunzo kuziba mapungufu na hatimayekutunukiwa vyeti ambavyo vitawawezesha kutambulika na kukubalika katika mfumo rasmi wa ajira.

Mh Mavunde aliongeza kuwa asilimia zaidi ya 68% ya watu hapa nchini ni vijana na ndio maana serikali imeamua kuandaa mpango huo na kuwekeza kwao hasa katika kuelekea katika uchumi wa viwanda kwani wao ndiyo nguvu kazi inayotegemewa.

Alisema miongoni mwa faida za programu hii ni kuwasaidia mafundi waliojifunza kupitia sehemu za kazi (wanagenzi) kupata kazi zenye staha na kuwajengea wanagenzi sio tu uwezo wa kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la ajira, lakini pia kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri/wenye makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.

Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA  Bi. Leah Dotto aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu  wa VETA wakati wa hafla hiyo ya ufunguzi, alisema  awamu ya tatu ya zoezi hili litahusisha mikoa mitano ambayo ni Morogoro, Dar es salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.

Alisema jumla ya wanagenzi 22,367 walijitokeza kufanyiwa tathimini ya ujuzi wao ambapo wanawake walikuwa 2,320 (sawa na 10.4%) na wanaume 20,047 (sawa na 89.6).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kati ya wanagenzi walioomba kufanyiwa tathmini ya ujuzi wao, jumla ya wanagenzi 14,424 (sawa na 64.5%) walikidhi vigezo vya kufanyiwa tathmini lakini kutokana na bajeti iliyopo, zoezi hilo litahusisha kuwafanyia tathmini wanagenzi 3,900 tu kati ya waliokidhi vigezo.

Aliiomba serikali kuwezesha zoezi hilo kuwafikia wanagenzi wengine wenye sifa waliowekwa kwenye orodha ya ziada (Reserve list).

Alisema VETA inatarajia kuongeza wigo wa mafundi wanaofanyiwa tathmini ya ujuzi ili kuwafikia mafundi katika nyanja nyingine kama Ushonaji, Ufundi bomba, Uungaji na Uundaji vyuma (Welding and Metal fabrication), urekebishaji wa bodi za magari (Auto body repair) na fani nyingine ambazo hazikuweza kufikiwa katika zoezi la awamu hii.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini Mh. Hawa Ghasia alisema ana uhakika kuwa baada ya mafunzo hayo ,vijana hao watakuwa chachu ya kukuza uchumi na hasa kukukuza fursa za ajira kwa vijana wa mkoa wa Mtwara.

Zoezi hilo ambalo lilianza tarehe 5 Januari 2017 limejumuisha fani za Ufundi Magari, Useremala, Uashi (ujenzi), Upishi na Uhudumu wa Hoteli na baa.


No comments:

Post a Comment