Vijana wenye
ualbino, pamoja na ulemavu mwingine wamehamasishwa kutumia fursa mbalimbali za elimu na mafunzo ya ufundi
stadi ili kupata ujuzi wa kuwasaidia kuajirika na kushiriki kikamilifu katika
kuchangia kwenye maendeleo ya kiuchumi nchini.
Akiwasilisha
mada kuhusu Fursa za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika warsha
iliyowakutanisha vijana wenye ualibino September 7, 2017, Afisa Uhusiano wa
VETA Dora Tesha alisema kuwa VETA imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha fursa
sawa za mafunzo kwa makundi yote kwenye jamii ikiwemo watu wenye mahitaji
maalum.
Alisema idadi
ya watu wenye ualbino katika vyuo vya ufundi stadi bado ipo chini huku takwimu
zikionesha kuwa kwa mwaka 2012 hadi 2016 idadi
ya watu wenye ulemavu
waliosajiliwa kwenye vyuo vya ufundi stadi walikuwa 4492 kati yao wenye ualbino
ni 420 pekee.
Alizitaja
baadhi ya sababu za udahili wa watu wenye ualbino kuwa wa chini kuwa ni pamoja
na kukosekana kwa uelewa kuwa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ni kwa makundi
yote ya jamii, ukosefu wa ujasiri kwa watu wenye ualbino na mtazamo wa jamii
juu ya kundi hilo kuingia kwenye mfumo rasmi wa ajira na kukosekana kwa watu wa
mfano (Role models) katika elimu ya ufundi stadi kutoka kwenye kundi hilo.
Naye, David
Edward Afisa Uhusiano pia kutoka VETA aliwasihi vijana wenye ualbino kuwa
mabalozi kwa wenzao juu ya umuhimu wa kujipatia ujuzi ili waweze kuendesha
maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.
Msimamizi wa warsha
hiyo kutoka shirika la Under The Same Sun Josephat Igembe alisema mada hiyo
imetoa mwanga na kufungua uelewa wa vijana hao juu ya fursa za kujipatia ujuzi
na kwamba wataitumia vyema.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Paskazia Yahaya kutoka mkoani Morogoro alisema kuwa mada ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imemsaidia kutambua kuwa fursa ya kujipatia ujuzi ni pana sana kwa kuwa si lazima mwanafunzi ahudhurie masomo chuoni kwani kuna njia nyingi za kutoa mafunzo.
“Nimehamasika sana kwenda VETA kupata
ujuzi ili niweze kujiajiri mwenyewe kwa kuwa changamoto ya kuajiriwa imekua
kubwa sana,” Alisema.
Warsha hiyo iliratibiwa
na shirika lisilo la kiserikali la Under the Same Sun kwa lengo la kuwajengea uelewa
vijana wenye ualbino nchini kuhusu masuala na mifumo mbalimbali ya kielimu na
ajira nchini na ilihudhuriwa na vijana zaidi ya 70 kutoka mikoa mbalimbali
nchini.
No comments:
Post a Comment