Mafunzo
ya mapishi na mapambo yaliyotolewa kwa vijana wilayani Kilombero, mkoani
Morogoro kupitia chuo cha VETA Mikumi, yamewasaidia vijana viziwi kujenga
ujasiri, hivyo kufungua mgahawa wa chakula unaotoa huduma katika mji wa
Ifakara.
Mafunzo
hayo yaliyotolewa chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) katika
kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2018 yalilenga katika kuwapatia
vijana, hususani wa makundi maalum mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha
kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri au kuajiriwa.
Ulemavu
wa kutosikia haujawazuia Bi. Elizabeth Lutta na Mwatanga Kibwana kutumia ujuzi
walioupata katika mafunzo hayo kwa kuanzisha mradi wa mgahawa wa kwao wenyewe.
Mgahawa
huo walioupa jina la EMFRANJO Catering and Decoration upo katikati ya mji wa
Ifakara na unavutia wengi kutokana na uwezo wanaoonyesha viziwi hao katika
mapishi na ukarimu wao katika kuhudumia wateja.
Pamoja na ulemavu walio nao, wameendelea
kupambana na ushindani wa kibiashara, jambo ambalo linashangaza wengi, hasa juu
ya namna ambavyo wanaweza kuwasiliana na kuelewana na wateja wao na kuwafanya
kufurahia na kuridhika na huduma zao.
Bi Lutta anasema mwanzoni ilikuwa tabu sana
wateja kuelewana nao kwa kuwa wao wanatumia lugha ya alama ambayo watu wengi
hawaifahamu, lakini walimudu changamoto hiyo kwa kutumia njia mbalimbali na kwa
sasa watu wengi wanaofika kupata huduma wanafahamu kuwa hawasikii na hivyo
hutumia mbinu mbalimbali kuwasiliana nao, ikiwemo kuandika au kuonesha picha za
huduma wanazohitaji.
“Ilikuwa
ngumu watu kuamini kuwa wanaweza kuhudumiwa na watu wenye changamoto ya usikivu
kama sisi, lakini baada ya muda watu wametuamini na wanakuja kupata huduma
kwetu kwa kuwa tunajitahidi kupika chakula kizuri na kuonesha huduma bora kwa
wateja wetu”Anasema
Kwa
upande wake Bi. Mwatanga Kibwana anasema baada ya kuanza biashara hiyo kwenye
kikundi anaweza kumudu mahitaji yake na kuchangia mahitaji ya familia yake tofauti
na ilivyokuwa mwanzoni kabla ya kupata mafunzo.
Anasema
wanaiona biashara yao ikiendelea kwa mafanikio kwani wanaaminika na wameanza
kupata zabuni za kuhudumia katika vikao mbalimbali hasa vya serikali za kata,
halmashauri na vyama.
Meneja
wa Mradi wa YEE Ifakara Bw Majani Rwambali anasema mradi huo umeonesha
mafanikio makubwa kwa kuwafikia na
kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi jumla ya vijana 1470 wa wilaya hiyo ambapo
wengi wao wameweza kujiajiri na wengine wameajiriwa.
Mafunzo
hayo yalihusisha fani za ushonaji, useremala, ujenzi, uchomeleaji, mapishi na
mapambo, ufundi simu, umeme, pamoja na udereva na ufundi wa magari.
Mradi
wa YEE ulianza mwaka 2015 kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya na unatekelezwa kwa
ushirkiano kati ya VETA, Plan International na asasi za CODERT na UHIKI.
No comments:
Post a Comment