Bodi mpya ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board) imedhamiria kuongeza nguvu katika
kuboresha na kupanua wigo wa utoaji Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.
Akizungumza
wakati wa semina ya kutambulisha shughuli za VETA kwa wajumbe wapya wa bodi ya
VETA tarehe 26 Mei, 2020, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Peter Maduki, ambaye pia
aliongoza Bodi iliyopita (2016 - 2019), amesema kuwa Bodi hiyo itahakikisha
kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi
ili kuchangia katika kujenga uchumi wa nchi.
Alisema ana
imani kuwa Bodi hiyo itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa, hasa kwa
kuwa Bodi hiyo imeundwa kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wadau wote muhimu wa
mafunzo ya ufundi stadi kama vile waajiri, waajiriwa, watoa mafunzo na watunga
sera.
“Waajiri
watatupa mrejesho wa jinsi wahitimu wa VETA wanavyofanya kazi na kutoa mwelekeo
wa aina ya mafundi stadi wanaowahitaji kwa siku zijazo na hivyo kutusaidia
kuandaa mafundi stadi watakaokidhi mahitaji ya waajiri hao”. Alisema
Amewasihi
wajumbe hao wa Bodi kufanya kazi kwa bidii, umakini, weledi na kutumia talanta
zao katika kuleta matokeo chanya zaidi kwenye elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Naye
Mwenyekiti wa RAAWU Taifa, Dkt. Michael Mawondo, ambaye pia ni mjumbe wa bodi
hiyo amesema kuwa Elimu ya Ufundi Stadi ni eneo muhimu sana katika maendeleo ya
kiuchumi na kijamii, kwani ndipo mahali inapozalishwa nguvukazi yenye ujuzi
unaozingatia mahitaji halisi ya soko kwa kada hiyo. Alisisitiza kuwa mikakati
zaidi inahitajika ili kuboresha utoaji wa mafunzo hayo.
Rais wa Chama
cha Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania, TCCIA Bw. Paul Koyi, ambaye pia
ni mjumbe wa Bodi hiyo, amesisitiza umuhimu wa VETA kuwekeza zaidi kwenye matumizi ya TEHAMA kwenye utoaji wa
mafunzo ili kuwezesha wahitimu wa ufundi stadi kuendana na mazingira halisi ya
mabadiliko ya teknolojia yanayoenda kwa kasi sana.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema kuwa VETA inaendelea na jitihada
mbalimbali za kupanua wigo wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuyafikia
makundi mbalimbali katika jamii na kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza tija
katika viwanda na kuboresha uzalishaji mali na huduma katika jamii.
Dkt. Bujulu
ameahidi kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa Bodi hiyo na kusisitiza kuwa
menejimenti ya VETA itafanyia kazi kwa umakini maelekezo yatakayotolewa na Bodi
hiyo.
Bodi hiyo
itahudumu kwa muda wa miaka mitatu (2020 – 2023) na wajumbe wake ni Bw. Peter
Maduki (Mwenyekiti), Bw.Ally A. Msaki (Mkurugenzi wa Ajira, Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Dkt. Ethel Kasembe (Naibu
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia), Dkt. Michael
Mawondo (Mwenyekiti wa RAAWU Taifa), Padre Dkt. Francis Xavier Ng’atigwa
(Mjumbe wa Baraza la Maaskofu Tanzania) na Bi. Clotilda Timothy Ndezi
(Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Uhamasishaji, Jumuiya Ya Kikristo
Tanzania, CCT).
Wengine ni Bw.
Nuhu Mruma (Katibu mkuu, BAKWATA), Bi. Anna Kimaro (Mtaalamu wa Sera za
Mazingira ya Biashara, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, CTI), Bw. Paul Faraj Koyi (Rais wa Chama cha wenye
Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania, TCCIA), Bi. Leah Ulaya (Rais wa Chama cha
Walimu Tanzania, CWT) na Dkt. Pancras Bujulu (Mkurugenzi Mkuu wa VETA, ambaye
ni Katibu wa Bodi).
Baadhi ya
wajumbe wapya wa Bodi ya VETA walifuatilia mada mbalimbali kuhusu shughuli za
VETA wakati wa semina
|
Wajumbe wapya
wa Bodi ya VETA katika picha ya pamoja na Menejimenti ya VETA mara baada ya
kuhitimisha semina juu ya shughuli za VETA kwa wajumbe hao leo tarehe 26, Mei
2020
|
No comments:
Post a Comment