Bodi
ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board) imedhamiria kuongeza
nguvu katika kuboresha na kupanua wigo wa utoaji Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.
Mwenyekiti
wa Bodi hiyo Ndg. Peter Maduki, aliyeteuliwa kwa mara ya pili kuongoza Bodi hiyo, anasema kuwa
Bodi hiyo imedhamiria kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia na
kuwanufaisha wananchi wengi zaidi ili kuchangia katika kujenga uchumi wa nchi.
Anasema
ana imani kuwa Bodi hiyo itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa, hasa kwa
kuwa imeundwa kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wadau wote muhimu wa mafunzo ya
ufundi stadi kama vile waajiri, waajiriwa, watoa mafunzo na watunga sera.
“Waajiri
watatupa mrejesho wa jinsi wahitimu wa VETA wanavyofanya kazi na kutoa mwelekeo
wa aina ya mafundi stadi wanaowahitaji kwa siku zijazo na hivyo kutusaidia
kuandaa mafundi stadi watakaokidhi mahitaji ya waajiri hao”. Anasema
Ndg.
Maduki anawasihi wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii, umakini, weledi
na kutumia talanta zao katika kuleta matokeo chanya zaidi kwenye elimu na
mafunzo ya ufundi stadi.
Mnamo
tarehe 8, Juni 2020, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce
Ndalichako, aliizindua rasmi Bodi hiyo na kuiagiza kuhakikisha mafunzo ya
ufundi stadi yanawafikia Watanzania wengi zaidi ili kutatua changamoto ya ajira
kwa vijana na kuchochea kasi ya uanzishwaji wa viwanda nchini.
Prof.
Ndalichako alisema kuwa elimu na mafunzo ya ufundi
stadi ni moja ya maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele na kutiliwa mkazo
zaidi katika kujenga uchumi wa viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu
ya Tano ya kujenga uchumi wa Viwanda.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, anasema kuwa VETA inaendelea na jitihada
mbalimbali za kupanua wigo wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuyafikia
makundi mbalimbali katika jamii na kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza tija
katika viwanda na kuboresha uzalishaji mali na huduma katika jamii.
Bodi ya
Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi itahudumu kwa muda wa miaka mitatu
(2020 – 2023) na wajumbe wake ni Ndg. Peter Maduki (Mwenyekiti), Ndg.Ally A.
Msaki (Mkurugenzi wa Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu
Wenye Ulemavu); Dkt. Ethel Kasembe (Naibu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia); Dkt. Michael
Mawondo (Mwenyekiti wa RAAWU Taifa); Padre Dkt. Francis Xavier Ng’atigwa
(Mjumbe kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania) na Bi. Clotilda Timothy Ndezi
(Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Uhamasishaji, Jumuiya Ya Kikristo
Tanzania, CCT).
Wengine ni
Ndg. Nuhu Mruma (Katibu mkuu, BAKWATA); Bi. Anna Kimaro (Mtaalamu wa Sera za
Mazingira ya Biashara, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, CTI); Ndg. Paul
Faraj Koyi (Rais wa Chama cha wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania,
TCCIA); Bi. Leah Ulaya (Rais wa Chama cha Walimu Tanzania, CWT) na Dkt. Pancras
Bujulu (Mkurugenzi Mkuu wa VETA, ambaye ni Katibu wa Bodi).
No comments:
Post a Comment