Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi imeendelea kusogeza
zaidi huduma za mafunzo kwa wananchi kupitia ujenzi wa vyuo vipya katika ngazi
ya wilaya na halmashauri.
Juhudi hizo zimeendelea kujidhihirisha kwa vyuo katika wilaya
mbalimbali kukamilika na kuzinduliwa rasmi miongoni mwake ikiwa ni Chuo cha
VETA Nyamidaho (wilayani Kasulu), VETA Nkasi na VETA Ileje.
VETA iliuaga mwezi Juni na kuukaribisha mwezi Julai kwa uzinduzi
wa vyuo vipya katika wilaya za Kasulu, Nkasi na Ileje ambapo Chuo cha Ufundi
Stadi Nyamidaho (VETA Nyamidaho) wilayani Kasulu kilizinduliwa tarehe 29 Juni,
2020, Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Nkasi (VETA Nkasi) tarehe 2 Julai,
2020 na Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ileje (VETA Ileje) tarehe 3 Julai,
2020.
Vyuo hivyo vilizinduliwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alieleza kuwa ukamilishaji
wa vyuo hivyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika kila Wilaya nchini ili kuhakikisha
mafunzo ya ufundi stadi yanafika karibu zaidi na wananchi.
Alisema katika mwaka wa
fedha 2019/20, Serikali ilikamilika ujenzi wa vyuo 10 katika Wilaya za
Namtumbo, Urambo, Ndolage, Nkasi, Ileje, Kanadi, Chato, Samunge, Gorowa na Mabalanga.
Waziri
Ndalichako aliwataka wananchi wa Wilaya za Kasulu, Nkasi na Ileje kutumia vyuo
hivyo kujipatia ujuzi ili kuweza kushiriki kikamilifu kuijenga Tanzania ya
viwanda hasa kwa kujiajiri kwa kufungua viwanda vidogo vidogo katika Wilaya zao
na kuajiri watu wengine.
“Mafunzo ya ufundi stadi ni mkombozi mkubwa katika kukabiliana na
tatizo la ajira, kwani ujuzi wa ufundi stadi unampa mhitimu fursa ya kuajiriwa
na kujiajiri,” alisema.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa vyuo
hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.
Pancras Bujulu alisema uwezo wa kudahili wanafunzi wa kozi za muda mrefu wa
VETA Nyamidaho ni 160, VETA Nkasi 160 na VETA Ileje 120, hivyo kwa pamoja vyuo hivyo vina uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 440 kwa mafunzo ya muda
mrefu, wakati kwa upande wa kozi za muda mfupi ni wanafunzi 1000.
Fani zitakazotolewa katika vyuo hivyo kwenye mabano ni VETA
Nyamidaho (Uashi, Ushonaji, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, na Umeme wa Majumbani);
VETA Nkasi (Ushonaji, Uhazili na
Matumizi ya Kompyuta, Umeme wa Majumbani
na Bidhaa za Ngozi) na VETA Ileje (Ushonaji, Uhazili na Matumizi ya
Kompyuta, na Umeme wa Majumbani).
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Peter
Maduki alishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa vyuo vya
ufundi stadi na kuagiza uongozi wa VETA kutoa mafunzo ya muda mfupi ya fani ya
Uashi bure kwa wananchi wanaohitaji mafunzo hayo katika kata ya Nyamidaho.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo alishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kukamilisha ujenzi wa
chuo cha VETA Nkasi na kuwataka wananchi wa Nkasi kutumia vyema chuo hicho
kujipatia ujuzi na kuleta maendeleo mkoani hapo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Bregedia Jenerali
Nicodemus Mwangela alisema kuwa chuo cha VETA Ileje kitakuwa mkombozi mkubwa
sana kwa vijana ambao wamekuwa wakihitaji mafunzo kwa ajili ya kujipatia ujuzi
kwenye fani mbalimbali.
No comments:
Post a Comment