Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea
kung’ara katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (maarufu kama
Sabasaba) ambapo licha ya kuvutia watu wengi kutembelea banda lake, VETA imeibuka mshindi wa tatu
katika kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi kwenye maonesho hayo ya 44 yaliyofanyika
jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 1 hadi 13 Julai 2020.
Katika Maonesho hayo, VETA ilionesha fursa za mafunzo ya
ufundi stadi, bidhaa, ubunifu pamoja na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na
walimu, wanafunzi na wahitimu wake ili kutatua changamoto mbalimbali kwenye
jamii.
Mshindi wa kwanza kwenye kundi la Elimu, Utafiti na
Uendelezaji Ujuzi ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nafasi ya pili
ilichukuliwa na Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Baadhi ya ubunifu
uliokuwa kivutio zaidi kwa watembeleaji wa maonesho hayo ni mashine ya kuzidua
Unga wa Ubuyu inayoendeshwa kwa umeme, Mfumo wa kielektoniki unaowezesha umeme
kuingizwa kwenye mita za umeme baada ya kulipia kwa njia ya simu, Meza ya kupasha
moto Chakula na Kupoza Vinywaji, Mtambo wa kuchemsha maji pasipo kutumia umeme,
kochi linaloweza kubadilika kuwa kitanda, vifaa vya umwagiliaji na kifaa cha
kurahisisha kupanda mbegu shambani.
VETA pia ilionesha namna
ilivyochangia katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu
unaosababishwa na Virusi vya Corona, (COVID 19 kwa kutengeneza vitakasa mikono, sabuni za maji, mashine za
kunawia mikono na barakoa.
Katika maonesho hayo, VETA
ilitembelewa na jumla ya wananchi 7,448, wakiwemo viongozi wa kitaifa wengi wao
walifurahishwa na kupongeza juhudi zinazofanywa na VETA hasa katika kupunguza
tatizo la ajira kwa vijana nchini huku wakishauri kutanua wigo wa utoaji
mafunzo ya ufundi stadi ili kufikia makundi mengi zaidi.
Miongoni mwawageni waliotembelea
Banda la VETA ni Katibu wa Bunge Ndg. Stephen Kagaigai ambaye alisifia VETA kwa
kuwa na teknolojia nzuri za ubunifu wa hali ya juu na kuishauri VETA
kuwaimarisha zaidi vijana wanaopata mafunzo katika vyuo hivyo ili waweze
kushindana katika soko.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa ushindi
huo umetoa hamasa kwa VETA kuendelea
kuboresha zaidi utoaji mafunzo ya ufundi stadi na kuendeleza ubunifu na
teknolojia mbalimbali ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda
nchini.
Maonesho hayo yaliyoongozwa na kauli mbiu, “Maendeleo ya Viwanda kwa Ajira
na Biashara Endelevu (Industrialization for Job Creation and Sustainable
Development), yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, tarehe 2 Julai 2020, na kufungwa na Waziri
wa Biashara na Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Balozi Amina
Salum Ali.
Maonesho hayo yalihudhuriwa na Makampuni, Taasisi na Mashirika
yapatayo 2,880 ya ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment