Wanahabari
wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), wameahidi
kuhamasisha jamii juu ya mafunzo ya ufundi stadi kwa kuwa yana umuhimu mkubwa katika
kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kuchangia katika uchumi wa viwanda.
Akizungumza katika mkutano kati ya Wanahabari hao na Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.Pancras Bujulu, uliofanyika katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam tarehe 17 Oktoba 2020, Mwenyekiti wa DCPC Irene Mark amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa taarifa juu ya fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa jamii ili Watanzania, hasa vijana waweze kujipatia ujuzi utakaowawezesha kujipatia ajira.
“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na VETA kwa
karibu zaidi ili tuweze kupata taarifa za mara kwa mara juu ya mafunzo haya na kuhakikisha
taarifa sahihi juu ya mafunzo ya ufundi stadi zinawafikia wananchi na kuwahamasisha
kujiunga na mafunzo haya,” amesema.
Naye
Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Hussein Siyovelwa, ameishukuru VETA kwa kuendelea
kuthamini mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii juu ya mafunzo ya
ufundi stadi kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali ambapo hatua hiyo
imesaidia wanahabari hao kuzidi kufahamu kwa kina shughuli zinazofanywa na
VETA.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amewasihi waandishi hao kuendelea
kuandika, kutangaza na kueneza habari zinazohusu Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi nchini ili kusaidia umma kupata uelewa wa kutosha na kunufaika na fursa
zilizopo VETA.
“VETA inatamani kuona kila mara waandishi wakiandika,
kutangaza na kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, ili kusaidia umma kupata uelewa wa kutosha na kunufaika na huduma
zetu,”amesema.
Dkt. Bujulu amefafanua masuala mbalimbali juu ya VETA na mafunzo ya ufundi stadi kwa ujumla kwa waandishi hao ikiwemo utoaji wa mafunzo na fursa za mafunzo hayo kwa Watanzania, mchango wa VETA kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ubunifu na uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, na nafasi ya wanahabari kwa maendeleo na ustawi wa VETA.
Akizungumza juu ya umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi, Dkt. Bujulu amesema mafunzo ya ufundi stadi ni suluhisho la changamoto ya ajira kwa kuwa ujuzi unaopatikana humpa mhitimu fursa ya kuajiriwa na kujiajiri na kusisitiza kuwa mafunzo hayo ni nguzo muhimu kwa uchumi wa viwanda, hasa kwa kuzingatia kuwa mafundi stadi ndio waendeshaji wa moja kwa moja wa viwanda na shughuli mbalimbali za uzalishaji.
“Tukiwa na mafundi stadi mahiri, uzalishaji viwandani utakuwa wenye tija zaidi. Vilevile wahitimu hawa wataweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vya kati, wakajiajiri na hata kuajiri wengine,” Dkt Bujulu amesema.
Kuhusu kupanua fursa za mafunzo ya ufundi stadi nchini, Dkt. Bujulu amesema lengo la Serikali ni kuwa na Chuo cha VETA kila Wilaya ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya 29 katika Wilaya za Chunya, Kilindi, Korogwe, Ukerewe, Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa Vijijini, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama, Chemba, Ruangwa, Nyasa, Kongwa na Kasulu Mji. Miradi ya ujenzi wa vyuo vya mikoa ya Rukwa, Geita, Njombe na Kagera pia inaendelea.
Kwa
mujibu wa Dkt. Bujulu, kukamilika kwa ujenzi wa vyuo hivyo vipya, kutaongeza
udahili wa wanafunzi kutoka 700,000 hadi kufikia wanafunzi Milioni Moja
(1,000,000) kwa mwaka.
VETA is doing well, Congratulation DG, VETA Management and all VETA Employees for Job well done MashaaAllah
ReplyDeleteAbdallah Ngodu