CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Saturday 17 October 2020

Wanahabari waahidi kuhamasisha jamii juu ya mafunzo ya ufundi stadi

Wanahabari wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), wameahidi kuhamasisha jamii juu ya mafunzo ya ufundi stadi kwa kuwa yana umuhimu mkubwa katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kuchangia katika uchumi wa viwanda.

Akizungumza katika mkutano kati ya Wanahabari hao na Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.Pancras Bujulu, uliofanyika katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam tarehe 17 Oktoba 2020, Mwenyekiti wa DCPC Irene Mark amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa taarifa juu ya fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa jamii ili Watanzania, hasa vijana waweze kujipatia ujuzi utakaowawezesha kujipatia ajira.

 “Tunaahidi kuendelea kushirikiana na VETA kwa karibu zaidi ili tuweze kupata taarifa za mara kwa mara juu ya mafunzo haya na kuhakikisha taarifa sahihi juu ya mafunzo ya ufundi stadi zinawafikia wananchi na kuwahamasisha kujiunga na mafunzo haya,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Hussein Siyovelwa, ameishukuru VETA kwa kuendelea kuthamini mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii juu ya mafunzo ya ufundi stadi kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali ambapo hatua hiyo imesaidia wanahabari hao kuzidi kufahamu kwa kina shughuli zinazofanywa na VETA.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amewasihi waandishi hao kuendelea kuandika, kutangaza na kueneza habari zinazohusu Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini ili kusaidia umma kupata uelewa wa kutosha na kunufaika na fursa zilizopo VETA.

“VETA inatamani kuona kila mara waandishi wakiandika, kutangaza na kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ili kusaidia umma kupata uelewa wa kutosha na kunufaika na huduma zetu,”amesema.

Dkt. Bujulu amefafanua masuala mbalimbali juu ya VETA na mafunzo ya ufundi stadi kwa ujumla kwa waandishi hao ikiwemo utoaji wa mafunzo na fursa za mafunzo hayo kwa Watanzania, mchango wa VETA kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ubunifu na uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, na nafasi ya wanahabari kwa maendeleo na ustawi wa VETA.

Akizungumza juu ya umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi, Dkt. Bujulu amesema mafunzo ya ufundi stadi ni suluhisho la changamoto ya ajira kwa kuwa ujuzi unaopatikana humpa mhitimu fursa ya kuajiriwa na kujiajiri na kusisitiza kuwa mafunzo hayo ni nguzo muhimu kwa uchumi wa viwanda, hasa kwa kuzingatia kuwa mafundi stadi ndio waendeshaji wa moja kwa moja wa viwanda na shughuli mbalimbali za uzalishaji.

“Tukiwa na mafundi stadi mahiri, uzalishaji viwandani utakuwa wenye tija zaidi. Vilevile wahitimu hawa wataweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vya kati, wakajiajiri na hata kuajiri wengine,” Dkt Bujulu amesema.

Kuhusu kupanua fursa za mafunzo ya ufundi stadi nchini, Dkt. Bujulu amesema lengo la Serikali ni kuwa na Chuo cha VETA kila Wilaya ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya 29 katika Wilaya za Chunya, Kilindi, Korogwe, Ukerewe, Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa Vijijini, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama, Chemba, Ruangwa, Nyasa, Kongwa na Kasulu Mji. Miradi ya ujenzi wa vyuo vya mikoa ya Rukwa, Geita, Njombe na Kagera pia inaendelea.

Kwa mujibu wa Dkt. Bujulu, kukamilika kwa ujenzi wa vyuo hivyo vipya, kutaongeza udahili wa wanafunzi kutoka 700,000 hadi kufikia wanafunzi Milioni Moja (1,000,000) kwa mwaka. 



1 comment:

  1. VETA is doing well, Congratulation DG, VETA Management and all VETA Employees for Job well done MashaaAllah

    Abdallah Ngodu

    ReplyDelete