Kikao cha watendaji waandamizi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kilichokuwa kikifanyika katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salam jana, tarehe 29 Novemba 2020, kimehitimishwa kwa uzinduzi wa Mkataba wa Utoaji Huduma kwa Wateja (Client Service Charter) na Mwongozo wa Alama za Utambulisho wa Mamlaka (VETA Branding Guidelines).
Uzinduzi wa miongozo hiyo ulifanywa na
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, ambapo Kaimu Mkurugenzi wa
Rasilimali Watu na Utawala, Felix Staki na Wakurugenzi wa Kanda za VETA
walikabidhiwa nakala na kutakiwa kusimamia utekelezaji wa miongozo hiyo katika
maeneo yao ya kazi.
Akitoa maelezo kwa ufupi kabla ya uzinduzi, Meneja Uhusiano wa Mamlaka, Sitta Peter amesema kuwa Mkataba wa Utoaji Huduma kwa Wateja wa VETA unafafanua viwango na ubora wa huduma ambazo VETA inaahidi kuzitoa kwa wateja wake, muda utakaotumiwa na watumishi wa Mamlaka kutoa huduma hizo na majukumu na wajibu wa mteja na taasisi katika kutoa huduma hizo.
“Mkataba huu unatufungamanisha na
wateja wetu. Tunapaswa kutoa huduma kwa ubora ulioanishwa kwenye Mkataba huu na
katika namna inayowaridhisha wateja wetu,” amesema.
Amesema kwa ujumla mkataba huo utatumika kama kipimo mahsusi cha utendaji kazi na uwajibikaji kwa kuzingatia mahitaji ya wapokea huduma, kutokana na ukweli kuwa watumishi wote wa umma wanapaswa kuwajibika kwa umma.
Kwa upande mwingine, Peter amesema kuwa Mwongozo wa Alama za Utambulisho wa VETA (VETA Branding Guidelines) umeandaliwa ili kusaidia kuweka mfanano na viwango sawa vya mwonekano wa Mamlaka nchini kote.
Ameongeza kuwa awali kulikuwa na utofauti mwingi katika matumizi ya Alama za Mamlaka zikiwemo nembo, rangi na namna za uandaaji nyaraka na machapisho.
Kikao cha watendaji waandamizi wa VETA
kilijadili mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya ujenzi na upanuzi
wa vyuo vya VETA, usimamizi wa mafunzo, hali ya rasilimali watu, mipango na
usimamizi wa fedha pamoja na maandalizi ya Kongamano la Ufundi Stadi
lililopangwa kufanyika Januari 2021 jijini Dodoma.
Aidha, katika kikao hicho wawezeshaji
kutoka nje ya Mamlaka walitoa mada kuhusu Maadili katika Utumishi wa Umma na
Utekelezaji Miradi ya Ujenzi kwa Kutumia Rasilimali za Ndani (Force Account).
No comments:
Post a Comment