MBUNGE
wa jimbo la Makete, Festo Sanga ameahidi kufadhili vijana 10 kila mwaka kusoma
katika chuo cha ufundi cha VETA Makete na kuwataka wazazi kupeleka vijana wao
kwa wingi katika chuo hicho ili waweze kujifunza fani mbalimbali.
Sanga
ameyasema hayo Ijumaa tarehe 27 Novemba 2020, akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali
ya sita ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Makete (VETA Makete).
Sanga
alisikitishwa kuona mwamko mdogo wa wananchi wa Makete katika kujiunga na
mafunzo ya ufundi stadi licha ya kusogezewa karibu huduma hiyo ya mafunzo.
"inasikitisha
kuona kati ya wanafunzi 64 wanaohitimu leo, wanafunzi wanaotokea hapa Makete
hawafiki 10, zaidi ya 50 wanatoka nje ya Makete, Mara, Tukuyu, Tanga, Dar es
Salaam, Iringa na kwingineko. Tafsiri yake ni kushindwa kuitumia fursa hii sisi
Wanamakete. Nawaomba sana tuwalete vijana wetu hapa waje wasome,” amefafanua.
Sanga amesema kuwa Serikali imewekeza mabilioni ya fedha katika chuo hicho pekee cha VETA katika mkoa wa Njombe ili wananchi wa Wilaya ya Makete waweze kunufaika na fursa za mafunzo ya ufundi stadi, hivyo akawaomba kuitumia vyema fursa hiyo.
Sambamba
na hilo, Sanga ameahidi kueneza ufahamu kwa umma juu ya mafunzo yatolewayo na
VETA ikiwemo ukweli kuwa gharama zake ni nafuu na kwamba Watanzania wengi
wanaweza kuzimudu.
Akiwa
katika mahafali hayo, Sanga alijionea karakana na kushuhudia maonesho ya ujuzi
na umahiri wa wanafunzi katika fani mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa batiki,
sabuni, uashi, ufundi seremala na ufundi wa magari.
Mahafali
ya chuo cha VETA Makete ilihusisha wahitimu 64, miongoni mwao wavulana 52 na
wasichana 12, katika fani za Ushonaji, Ufundi wa Magari, Useremala na Uashi.
No comments:
Post a Comment