CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday, 25 November 2020

Wahitimu wa ufundi stadi wahamasishwa kuchangamkia fursa za mikopo kwenye halmashauri za wilaya

 


Wahitimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi wamehamasishwa kujiunga katika vikundi na kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa katika halmashauri za wilaya nchini ili waweze kujiajiri baada ya kupata ujuzi.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare katika mahafali ya Chuo cha VETA Kihonda, yaliyofanyika Ijumaa tarehe 20 Novemba 2020.

Amesema kila mwaka halmashauri zote nchini hutenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya kusaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, hivyo wahitimu wa VETA wana fursa nzuri za kunufaika na mikopo kwa kuanzisha vikundi na miradi yao.

Kwa upande mwingine, Waluse amewashauri wamiliki wa makampuni yenye magari makubwa kuwapeleka madereva wao kupata mafunzo ya umahiri kwenye chuo cha VETA Kihonda, kwani chuo hicho kimebobea sana katika kutoa mafunzo ya Udereva wa Magari Makubwa.

Mkuu wa Chuo hicho, Kashindye Maganga, amesema baada ya kubaini uhitaji wa mafunzo ya udereva wa magari makubwa na changamoto ya upatikanaji wa muda wa kuhudhuria mafunzo kwa madereva walio kazini, chuo hicho kimebuni utaratibu wa kuwafuata waliko (outreach) na kuendesha mafunzo kwenye maeneo yao.

Alisema utaratibu huo umekiwezesha chuo kufundisha madereva 1474 (wanaume 1463 na wanawake 11) katika kipindi cha kuanzia Januari 2019 hadi Novemba 2020.

Alisema kupitia mpango huo makampuni mengi yameitikia kutoa madereva wao kupata mafunzo na kuyataja baadhi ya makampuni hayo kuwa ni pamoja na World Oil, Mohamed Enterprises, GSM, Overland na TANCOAL Songea.


Mahafali hayo ilihusisha jumla ya wahitimu 241 katika fani  za Ufundi wa Zana za Kilimo, Ufundi Uashi, Ufundi wa Ushonaji Nguo  Ufundi Bomba, Ufundi Useremala, Ufundi wa Mafriji na Viyoyozi , Ufundi wa Umeme wa Majumbani, Ufundi wa Mitambo na Ukerezaji Vyuma, Ufundi wa  Magari na Ufundi wa Umeme wa Magari ambapo wahitimu  186 walikuwa ni wanaume na 55 wanawake.



No comments:

Post a Comment