Wadau
wa hoteli na utalii katika mikoa ya Lindi na Mtwara wameusifu Mpango wa Mafunzo
ya Uanagenzi Pacha (Dual Apprenticeship Training) unaoendeshwa na Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kusema kuwa umesaidia kwa kiasi
kikubwa kuongeza tija mahala pa kazi.
Wakizungumza wakati wa Semina Elekezi kwa Wasimamizi wa Sekta ya Hoteli na Utalii iliyoendeshwa na VETA katika ofisi ya VETA Kanda ya Kusini Mashariki iliyopo mkoani Mtwara, tarehe 16 Novemba 2020 wamiliki hao walisema mpango huo umekuwa na manufaa katika kampuni zao, kwani pia wanashiriki katika kuwafundisha wanagenzi (wanafunzi) waliopo katika mpango huo, hivyoi inasaidia kupata wafanyakazi bora.
Akichangia wakati wa semina hiyo, Meneja wa Tiffany Diamond Hotel, Nassoro Kingazi alisema mpango huo umekuwa na tija katika kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi kwenye maeneo yao ya kazi.
Aliwaomba wamiliki wengine wa hoteli kuunga mkono mpango huo kwa kuruhusu vijana kufanya mafunzo kwa vitendo katika hoteli zao ili wawe bora na kukubalika katika soko la ajira
“Kwangu mimi programu hii naichukulia kama uwezekaji mkubwa kwa wadau na ushirikiano mzuri kwa sababu tunakuwa na uhakika wa soko la ajira kwa wale vijana tunaokuwa tunawatengeneza na kuwaanda. Kupitia programu hii inatupa uhakika kwamba wanafunzi ambao wanakuwa wamefundishwa na vyuo vya VETA ni mtaji tosha kwetu kwa sababu tunakuwa tumewapika wenyewe na tunatambua kabisa zao hili halitapotea na ni la uhakika,” alisema.
Naye
Meneja wa Naf Beach Hotel, Fadhili
Mkwemba, aliishukuru VETA kwa kuanzisha Mpango huo ambao umemuwezesha
kushirikiana na chuo cha VETA Mtwara katika kutoa mafunzo kwa wanagenzi (wanafunzi).
Alisema wanagenzi hao wamekuwa mfano wa kuigwa katika idara zote nne za hoteli yake zikiwemo Mapokezi, Upishi, Usafi na Uhudumu Vyumbani na Huduma ya Chakula na Vinywaji.
Aliahidi kuwa hoteli yake itaendelea kupokea wanafunzi kutoka VETA ili wapate nafasi za mafunzo kwa vitendo ili kuwa mahiri zaidi.
Mratibu wa mpango huo, Francis Komba alisema kuwa semina hiyo imelenga kutoa majukumu kwa wasimamizi wa hoteli hizo juu ya mbinu bora za kushirikiana na wanagenzi, njia bora za kutoa mafunzo na viwango vya kuwapima uelewa wanagenzi hao hao.
Mwanagenzi kutoka Chuo cha VETA Mtwara Salma Masoud amewahimiza vijana kujiunga na mafunzo kupitia mpango wa uanagezi, kwani unasaidia kupata ujuzi na kuweza kuajirika.
Hoteli zilizoshiriki semina juu ya mpango huo wa mafunzo ya Uanagenzi Pacha katika mikoa ya Lindi na Mtwara ni pamoja na Tiffany Diamond hotel, Naf beach hotel pamoja na VETA CCC hotel.
Baada
ya semina hiyo elekezi kampuni hizo zimetoa ahadi ya kupokea wanagenzi ishirini
kwa mwendelezo wa Uanagenzi Pacha kwa mwaka wa masomo 2021.
No comments:
Post a Comment