Jumla ya mafundi 200
wa simu za mkononi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wanatarajia kunufaika
na mafunzo ya umahiri wa ufundi wa simu za mkononi yanayotolewa na Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Akizindua mafunzo
hayo jijini Arusha, tarehe 4 Desemba, 2020, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Idd
Hassan Kimanta, alisema mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuandaa mafundi simu
watakaofanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Mhe. Kimanta alisema
mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka ambapo matumizi ya simu za mkononi yanaendelea
kuongezeka kwa kasi kubwa na vijana wengi wanajipatia ajira kupitia shughuli za
ufundi simu hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha ujuzi wao na kuweza
kufanya kazi hizo kwa tija zaidi.
Mhe. Kimanta aliwataka mafundi hao kuzingatia mafunzo
yatakayotolewa ili wakafanye kazi kwa weledi kwa kuhakikisha usalama wa simu
watazotengeneza pamoja na usalama wa maisha ya watumiaji pamoja na mali zao.
Mafunzo hayo
yanatolewa na VETA kupitia vyuo vyake vya VETA Moshi na VETA Arusha kwa uratibu
wa Chuo cha Tehama VETA Kipawa, na kufadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA).
Mkurugenzi Mkuu wa
VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema uhitaji wa ujuzi wa ufundi simu ni mkubwa hasa
ukizingatia kuwa matumizi ya simu za mkononi Tanzania yameongezeka kwa kasi
kubwa ambapo hadi sasa zaidi ya simu za mikononi milioni 45 zinatumika sehemu
mbalimbali nchini, na zimeenea kwa zaidi ya asilimia 65 ya Tanzania.
Dkt. Bujulu alisema kanzidata
zimeonyesha kuwa kuna Watanzania zaidi ya 4,700 walioonyesha uhitaji wa mafunzo
hayo ambapo asilimia 10 ni wanawake na asilimia 3 wako kwenye kundi la watu
wenye uhitaji maalum.
“Mikoa inayoongoza
kwa uhitaji wa mafunzo haya ni pamoja na Dar es salaam 1,174; Dodoma 237;
Kigoma 168; Arusha 116; Kilimanjaro 130; Tanga 93 na Manyara 78. Pia mikoa kama
Iringa, Mtwara, Lindi, Ruvuma na Zanzibar imeonyesha uhitaji mkubwa kupata
mafunzo haya,”alisema.
Alisema VETA
itaendelea kuhakikisha mafunzo hayo yanatolewa kwa mafundi simu wenye uhitaji
nchini kote ili kuwezesha mafundi simu kujipatia ujuzi stahiki utakaowawezesha
kufanya kazi zao kwa umahiri zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa
TCRA Mhandisi James Kilaba alisema TCRA
itaendelea kufadhili utoaji wa mafunzo hayo ili kuhakikisha mikoa yote nchini
inafikiwa na mafunzo hayo muhimu.
Kwa mujibu wa
Mhandisi Kilaba, mafundi watakaofuzu mafunzo hayo watakidhi vigezo vya kupatiwa
leseni za uendeshaji wa ufundi wa simu za mkononi kutoka kwenye Mamlaka hiyo.
Hadi sasa jumla ya mafundi 295 wa simu za mkononi
wamekwishanufaika na mafunzo hayo ambapo 95 ni katika mkoa wa Dar es Salaam,
100 mkoa wa Dodoma na wengine 100 katika mkoa wa Kigoma. Mafunzo hayo
yalizinduliwa rasmi kitaifa tarehe 4 Septemba, 2020 jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment