Fursa zaidi za mafunzo ya ufundi stadi kwa wananchi mkoani Arusha zinatarajia kuongezeka baada ya kukamilika kwa miradi ya upanuzi wa vyuo viwili vya VETA mkoani hapo na ujenzi wa Chuo kipya cha VETA cha Wilaya ya Longido.
Akikagua maendeleo ya
ujenzi wa majengo mapya katika chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VETA Njiro)
na Chuo cha VETA Arusha, tarehe 5 Desemba, 2020, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu, amesema miradi ya
upanuzi wa vyuo hivyo umelenga kuongeza udahili wa wanafunzi na kuboresha
mazingira ya utoaji mafunzo.
Katika Chuo cha VETA
Njiro, Dkt. Bujulu amesema kazi ya ujenzi wa ukumbi wa mihadhara (lecture
theatre), madarasa mawili, maliwato pamoja na ukarabati wa majengo ya hoteli na
utawala inaendelea ambapo kiasi cha shilingi 647, 677,362 kimetengwa kwa kazi
hiyo.
Dkt. Bujulu
ameainisha majengo yanayojengwa katika chuo cha VETA Arusha kuwa ni Maabara ya
Kompyuta na Uhazili, karakana za Ufundi Magari na Uungaji Vyuma pamoja na bweni
la wasichana lenye uwezo wa kulaza wanafunzi wa kike 80 ambapo kiasi cha
shilingi milioni 604,533,040 kimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Msimamizi wa miradi
hiyo, Mhandisi Method Mlay, amesema miradi hiyo ya ujenzi inatarajiwa
kukamilika mwezi Machi, 2021 na kwamba ujenzi huo umefikia asilimia 60.
Katika hatua
nyingine, mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya ya Longido unaotekelezwa
na Chuo cha VETA Arusha kwa utaratibu wa kutumia rasilimali za ndani (Force
Account) unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Januari, 2021 na kuongeza fursa
zaidi za mafunzo ya ufundi stadi kwa wananchi wilayani hapo.
Dkt. Bujulu
aliwasisitiza viongozi wa chuo hicho kuhakikisha ujenzi unaenda kwa kasi ili
wananchi wa Wilaya hiyo waanze kunufaika na mafunzo na hatimaye kuendesha kwa
tija shughuli zao za kiuchumi.
Mkuu wa Chuo cha VETA
Arusha, Ndugu Bangantabona Mrefu, amesema chuo chake kitaendelea kuzidisha
jitihada ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora
uliokusudiwa.
Chuo cha VETA cha
Wilaya ya Longido ni miongoni mwa vyuo 26 vya VETA vya Wilaya vinavyojengwa
nchini ikiwa ni mkakati wa Serikali kuhakikisha kila Wilaya nchini inakuwa na
chuo cha VETA. Chuo cha VETA Longido kinajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni
1.7.
No comments:
Post a Comment