Wahitimu wa
Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma Dar es Salaam wametakiwa kuendeleza
bidii na moyo wa kujituma waliojengewa wakati wa masomo katika sehemu zao za
kazi ili waweze kufanikiwa.
Akizungumza
katika mahafali ya 50 ya Chuo hicho iliyofanyika tarehe 4 Desemba, 2020 jijini
Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Ndugu Deogratius
Lukomanya aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Godwin Gondwe, alisema ili
kijana aweze kufanikiwa akiwa kazini ni lazima kuweka bidii na hamasa ya
kujituma katika kazi zozote atazokuwa anazifanya.
Lukomanya
amewataka wahitimu hao kuondokana na dhana ya kusubiria kuajiriwa bali wajitume
kwa kujitengenezea ajira wao wenyewe ili waweze kutoa ajira kwa vijana wengine.
“Katika karne hii ya ishirini na moja, upatikanaji wa ajira umekuwa ni changamoto kubwa ulimwenguni kote, hivyo ni wajibu wenu kuwa na mawazo ya kujitengenezea ajira zenu wenyewe kwa ujuzi mliopata,” alisema.
Ndugu
Lukomanya aliwataka waajiri kuendelea kuwapokea wanafunzi na wahitimu wa VETA
katika viwanda na makampuni yao na kuwapa nafasi za mafunzo kwa vitendo pamoja
na ajira pale zinapopatikana.
Mkuu wa Chuo
cha VETA Dar es Salaam, Bw. Joseph Mwanda, alisema kwa mwaka 2020, jumla ya
vijana 616 wamehitimu masomo yao katika kozi za ufundi stadi katika ngazi ya
pili (Level II), ngazi ya tatu (Level III) na ngazi ya Diploma.
Alisema chuo
hicho kimeweza kusajili jumla ya wanafunzi 1,361 kwa kozi za muda mrefu na
10,808 kwa kozi za muda mfupi kwa kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Oktoba
2020.
Kwa mujibu wa
Ndugu Mwanda, chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya ufundi stadi kwa wanafunzi
wenye mahitaji maalum ambapo kwa mwaka 2020 jumla ya wanafunzi 21 wenye
mahitaji maalum wamesajiliwa katika fani za uungaji vyuma na ushonaji.
"Kati ya
wanafunzi tuliowasajiliwa wenye mahitaji maalum, kumi ni wenye ulemavu wa mfumo
wa akili na wengine kumi na moja wana ulemavu wa viungo ambapo wengi wao
wameonyesha uwezo mkubwa kwenye masomo yao,”alisema.
Mwanda alisema
vijana hao wamekuwa wakionyesha uwezo mkubwa kwenye masomo yao huku akitoa
mfano wa mhitimu Neema Eliasi Chole wa fani ya ushonaji ambaye amekuwa akifanya
vizuri katika masomo yake na kupata wastani wa alama ‘B’ katika mtihani wa Taifa na hatimaye chuo kuamua
kumzawadia Cherehani kwa kutambua jitihada zake na kumwezesha kujiajiri.
Akizungumza
kwa niaba ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo, Bi. Aveline Mrema amewahimiza
wahitimu kutokata tamaa katika maisha
yao kwani ukarasa mpya wa maisha umeanza ambapo wahitimu hao wanaweza kukumbana na changamoto mbalimbali
wanapoingia kwenye soko la ajira.
Naye mwakilishi wa waajiri kutoka kampuni ya Reveurse Tanzania Limited, Bi. Njile Bwana, alipongeza VETA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kukuza ujuzi kwa vijana ambapo alisema kupitia kampuni yake inayoshughulika na ajira, kampuni nne zimeonesha nia ya kuchukua wahitimu wa VETA hali inayoonyesha ni kwa namna gani vijana wa VETA ni bora.
No comments:
Post a Comment