Imebainika kuwa
matumizi ya vifungashio duni kwa wakulima wa nyanya ni chanzo cha upotevu wa
mavuno ya zao hilo.
Utafiti uliofanywa na
Mwalimu wa fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo (Agro –Mechanics) VETA Kihonda,
Mhandisi Joseph Kimako umebainisha kuwa wakulima wengi wa nyanya nchini
wanatumia makasha ya mbao ambayo husababisha uharibifu mkubwa wa nyanya wakati
wa usafirishaji.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti juu ya upotevu wa mavuno katika zao la nyanya (Assessment of Post-harvest losses in tomato production) katika mkutano wa 12 wa Kimataifa wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), uliofanyika tarehe 3 hadi 5 Desemba, 2020, Mhandisi Kimako alisema utafiti utafiti alioufanya katika wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro umeonyesha kuwa asilimia 63 ya wakulima hutumia makasha ya mbao kusafirisha nyanya kwenda kwenye masoko huku asilimia 37 pekee ya wakulima hutumia makasha ya plastiki. Kasha za plastiki ni salama zaidi kwa kuwa ni laini na huruhusu hewa kupita kirahisi na hatimaye kuzuia uharibifu kwenye nyanya.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kimako, robo ya
nyanya zinaharibika baada ya kuvunwa kutokana na changamoto ya vifungashio
inayosababishwa na uwezo mdogo wa kiuchumi kwa wakulima kuweza kununua makasha
ya plastiki na changamoto ya upatikanaji wa kreti hizo katika maeneo yao.
Sababu zingine
zinazosababisha upotevu wa zao hilo kwa mujibu wa utafiti huo ni pamoja na
ukosefu wa soko la uhakika la zao hilo mara baada ya mavuno na ukosefu wa elimu
ya namna bora ya kupunguza upotevu wa nyanya baada ya kuvuna.
Utafiti huo umeainisha
mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo ambayo ni pamoja na ujenzi
wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika nyanya katika maeneo yanayolimwa zao
hilo, mafunzo kwa wakulima juu ya namna ya kupunguza upotevu wa nyanya wakati
wa kilimo na baada ya mavuno pamoja na ujuzi wa kukabiliana na upotevu wa
mazao.
Mhandisi Kimako alisema VETA itaendelea kuwasaidia wakulima kwa kuwashauri namna bora ya kupunguza hasara zinazotokana na upotevu wa zao la nyanya kabla na baada ya mavuno pamoja na kubuni vifaa na teknolojia mbalimbali za kusaidia kupunguza changamoto hiyo.
No comments:
Post a Comment