CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 25 May 2021

HAFLA ya makabidhiano ya vifaa vya mafunzo ya stadi za Uvuvi na Uchakataji wa Samaki kwa ajili ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

 

HAFLA ya makabidhiano ya vifaa vya mafunzo ya stadi za Uvuvi na Uchakataji wa Samaki kwa ajili ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Wageni Rasmi katika hafla hiyo walikuwa ni Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mheshimiwa Wang Ke, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania.

Viongozi na watendaji wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Dkt. Leonard Akwilapo, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Dkt. Ethel Kasembe, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Elimu ya Ufundi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Ndugu Peter Maduki, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi; Wakurugenzi na Menejimenti ya Makao Makuu pamoja na Wakuu wa vyuo vya VETA vya Chato, Kipawa na Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu ndiye aliyekuwa mwenyeji wa tukio hilo.


Vifaa vilivyokabidhiwa leo vinatokana na ahadi iliyotolewa tarehe 7 Januari 2021 na Mheshimiwa Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje ya China na Mjumbe wa Baraza la Taifa la nchi hiyo wakati wa Uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato. Kwa niaba ya Serikali yake, Mheshimiwa Yi aliahidi kutoa kiasi cha Yuan milioni moja karibu sawa na shilingi milioni 350 kwa ajili ya kununua vifaa vya Mafunzo ya Stadi za Uvuvi na Uchakataji Samaki kwa ajili ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato.

Mheshimiwa Waziri amesema, “Msaada huu ni muhimu sana na wa kipekee kwani unakwenda kuchangia katika kozi ambayo ni mpya kwenye mafunzo ya ufundi stadi. Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato kitakuwa chuo cha kwanza kabisa kuanza kutoa mafunzo ya Ufundi Stadi kwenye eneo la Uvuvi na Uchakataji wa Samaki.

Matarajio ni kuwa mafunzo hayo yatawasaidia sana wananchi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria kuboresha shughuli zao za kiuchumi ambazo zinahusiana zaidi na uvuvi na biashara ya samaki. Miongoni mwa manufaa yanayotarajiwa ni kuongeza mavuno ya samaki na kuongeza thamani ya samaki na mazao yake.

Ameishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, hususani ile inayolenga kuboresha uendelezaji ujuzi na sekta ya elimu kwa ujumla.

Naye Balozi wa China nchini, Wang Ke, amesema Serikali yake itaendelea kusaidia miradi mbalimbali ya elimu nchini kwani inatambua kuwa elimu ina mchango mkubwa sana katika kuongeza tija na kuchangia maendeleo ya taifa.

 

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, katika mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya hafla ya makabidhiano ya vifaa vya Mafunzo ya Uvuvi na Uchakataji wa Samaki vilivyotolewa kwa msaada wa Serikali ya China. Tukio la makabidhiano lilifanyika, tarehe 25 Mei 2021, VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

 
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu akiwapitisha Mheshimiwa Waziri, Balozi na viongozi wengine kwenye eneo lililopangwa vifaa mbalimbali vilivyonunuliwa kwa msaada huo wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia (kulia) na Mhe. Wang Ke, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini (kushoto) wakionesha nyaraka za makabidhiano baada ya kutia saini.  Wanaoshuhudia nyuma kutoka kushoto ni Ndugu Peter Maduki, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Stadi; Dkt. Pancras Bujulu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA; Ramadhani Sebbo, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato na Dkt. Leonard Akwilapo, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
 
 

No comments:

Post a Comment