Jumbe Haruni Jumbe ni mhitimu wa VETA katika fani ya Ufundi Bomba kutoka Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Kihonda. Alihitimu mwaka 1997 na kuamua kujiajiri..
“Ilikuwa mwaka 1998
ambapo wazazi wangu waliniwezesha vifaa vya kufanyia kazi nikaingia mtaani
kufanya kazi za ufundi bomba na uchomeleaji na hatimaye nikaweza kuanzisha
kijiwe changu maeneo ya nyumbani kwetu Mzumbe mkoani Morogoro” Anasema.
Anasema mwaka 2003 alihama kutoka Mzumbe na kuelekea
Mikumi, Morogoro ambako aliendelea na shughuli hizo za ufundi kwa
kufungua karakana rasmi. Mafanikio aliyoyapata kupitia karakana yake,
yalimwezesha kufungua kampuni yake ya Jumbe Plumbers and General Maintenance na
kuisajili rasmi mwezi Septemba 2007.
“Juhudi, maarifa, uaminifu
na kuipenda kazi yako kwa kuifanya kwa wakati na kama
alivyokubaliana na
wateja wako, ndo kunakokuchangia kwa kiasi kikubwa kukufanya upate wateja
wengi, kujulikana na kudumu katika
biashara yako,” anasema.
Licha ya kupata
mafanikio katika shughuli zake, Jumbe anasema katika karakana yake amesaidia vijana wengi kujifunza ufundi
na hata kuajiri wengine. Kwa sasa
ameajiri vijana wanne.
“Nilipokea vijana
wa aina mbalimbali na kuwafunza ufundi bomba na kuchomelea vyuma... Vijana hawa
walipenda kujifunza lakini wazazi wao hawakuwa na uwezo kuwapeleka VETA,”
Anasema.
Pamoja na ujuzi na uzoefu katika kazi za Ufundi Bomba,
Jumbe alifanikiwa kubuni mifumo mbalimbali ya kuwezesha upatikanaji wa maji
moto kwa kutumia nishati ya jua, ubunifu ambao umemwezesha kushinda
katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU)
mwaka 2019.
Hata hivyo Jumbe anasema hajaweza kupata fursa pana ya
kujitangaza ili kupata soko la bidhaa za kibunifu kufikia watu wengi zaidi
ndani na nje ya nchi.
Jumbe anawashauri vijana nchini kujiunga na mafunzo ya
Ufundi Stadi kwani yatawawezesha kuajiriwa au kujiajiri wao wenyewe na vijana
wenzao.
No comments:
Post a Comment