Yuda Basil Temba
alizaliwa mnamo mwaka 1980 na kujiunga na Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Moshi
(VETA Moshi) katika fani ya Ufundi wa Umeme wa Majumbani (Electrical
Installation) na baadaye Chuo cha Ufundi
Stadi Arusha (VETA Arusha-Oljoro) katika fani ya Ufundi wa Umeme wa Magari (Auto
electrical).
Baada ya kumaliza
chuo alifanikiwa kufanya kazi katika viwanda na migodi ikiwemo Buzwagi na Geita
Gold Mining.
Kutokana na ujuzi
na uzoefu alioupata chuoni na katika viwanda na migodi hiyo, Temba alipata mawazo ya kubuni vitu mbalimbali vya kusaidia
utendaji kazi katika viwanda mfano mashine za kusaga mawe (crusher) na za
kuchenjua dhahabu.
Temba anasema kupitia
ubunifu huo, aliweza kujikwamua na tatizo la ajira ambapo alifanikiwa kufungua
duka la vifaa vya umeme na kubuni saketi mbalimbali za viwandani mkoani Geita. Baadaye,
alifanikiwa kufungua karakana ndogo mkoani Geita na kuajiri vijana tisa, watatu kati yao wakiwa ni wahitimu wa
VETA.
Baada ya karakana
hiyo kufanya vizuri, alifanikiwa kufungua kampuni inayojishughulisha na
utengezaji wa mashine za Elution za kuchenjulia dhahabu kwa wachimbaji wadogo
na wa kati, mashine ambazo aliweza
kuzifunga ndani na nje ya
nchi kama vile DR Congo na Mauritania.
Temba
anaishukuru VETA kwani licha
ya kumuwezesha kupata ujuzi na umahiri katika ufundi stadi pia alifanikiwa
kuingia kwenye Mashindano ya
Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu( MAKISATU 2020) ambapo alifanikiwa
kuwa mshindi wa tatu katika kundi la Wabunifu wa Vyuo vya Ufundi
stadi.
Anawashauri vijana
wote na wahitimu wote wa vyuo mbalimbali kujifunza ufundi stadi ili kuwakwamua
katika tatizo la ajira. Pia anaiomba serikali kuwawezesha wabunifu ili kuleta mabadiliko
ya haraka kwenye sekta ya viwanda.
No comments:
Post a Comment