Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
Ndg. Ali Zubeiry, ameridhishwa na hatua za ujenzi wa vyuo vya Ufundi Stadi vya
Wilaya za Pangani, Mkinga na Korogwe mkoani Tanga.
AAG ameeleza hayo leo tarehe 24 Oktoba, 2022 wilayani Korogwe wakati akihitimisha ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyuo hivyo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kutumia utaratibu wa nguvu kazi ya ndani yaani force account.
"nimetembelea na kujionea namna VETA ilivyotekeleza miradi hii na nikiri wazi kuwa nimeridhishwa na utekelezaji wa miradi hii...nimejionea vyuo ni vikubwa, majengo imara na ni ya kiwango hivyo naamini wananchi watanufaika na vyuo hivi,"amesema
Ndugu Zubeiry ameitaka VETA kuhakikisha inaweka miundombinu ya maji kupitia vyanzo vya maji vya uhakika na vya kudumu ili kuwezesha upatikanaji wa maji ya kutosheleza wanafunzi na wafanyakazi watakaotumia vyuo hivyo.
Awali, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Ndugu Wilhard Soko, alimjulisha AAG kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha Wilaya ya Korogwe umefikia asilimia 95 na kwamba mafunzo yanatarajia kuanza mwezi Januari, 2023.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda ambaye ni mtekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Korogwe, Bi Theresia Ibrahim, amesema chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 300 wa kozi za muda mrefu na wengine zaidi ya 1000 kwa kozi za muda mfupi.
Amezitaja kozi zitakazotolewa kwenye chuo hicho
kuwa ni Ufundi Umeme, Ufundi Magari, Uchomeleaji na Uungaji Vyuma, Uashi,
Ushonaji pamoja na Uhazili na Kompyuta.
No comments:
Post a Comment