CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday, 21 October 2022

TAKUKURU YAIPONGEZA VETA UJENZI WA CHUO CHA UFUNDI STADI CHA WILAYA YA IKUNGI

 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) imeipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kutekeleza kwa ufanisi mradi wa ujenzi wa  ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha VETA Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye, ametoa pongezi hizo tarehe 19 Oktoba, 2022 wakati wa ziara ya siku moja ya kutembelea chuo hicho akiongozana na  viongozi wa Wilaya ya Ikungi wakiwepo wajumbe wa kamati ya ulizi na usalama wa wilaya kukagua ujenzi wa chuo hicho unaofanywa na Ofisi ya VETA Kanda ya kati.

 “Nifaraja nimekuja na kuona hatua mliyofikia majengo mliyojenga na miundombinu ipo katika viwango tarajiwa vinavyotakiwa na Serikali na hilo nalo ni sababu nyingine ya kuwapongeza wale wote mlioufikisha ujenzi huu katika hatua hii nzuri licha ya mradi kuwa na changamoto,” alisema Mwakalyelye.

Bi Mwakalyelye aliitaka VETA kuendelea kutekeleza kwa ufanisi miradi mingine ya ujenzi inayotekelezwa nchi nzima na kutumia miradi hiyo kama sehemu ya kujenga uwezo kwa wafanyakazi wa wataalamu wake wa ndani.

 “Nimtake Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma John Mwanja ampelekee ujumbe huu Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini kuona kwamba miradi kama hii inayofanywa vizuri itumike kama miradi ya mafunzo ya ndani kwa ajili ya kujengeana uwezo katika maeneo mengine ambayo miradi ya namna hiyo inapelekwa,” alisema Mwakalyelye.

Awali, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati John Mwanja akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo hicho alisema Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi chenye umiliki wa Hati namba: 2218- SGD kinajengwa katika Kijiji cha Muungano,Kata ya Unyahati wilayani Ikungi katika mkoa wa Singida kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 50.

Alisema Mradi huo ulianza mwezi Machi, 2020 ukisimamiwa na chuo cha VETA Singida na ulipaswa kutekelezwa kwa muda wa miezi sita hata hivyo, haukuweza kukamilika kwa wakati kutokana na changamoto kadhaa zilizojitokeza na baadaye mradi kusimama kwa muda wa mwaka mmoja.

Alisema mwezi 2022 majukumu ya usimamizi wa Ujenzi wa chuo hicho yalihamishwa kutoka Chuo cha VETA Singida kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa VETA Kanda ya kati ambaye hadi sasa ndiye anaendelea na usimamizi wa ujenzi huo ambao unatekelezwa kwa mfumo wa “Force Account”.

Alisema mradi huo unahusisha jumla ya majengo 17 ambayo ni Jengo moja la utawala, Majengo manne ya karakana, jengo moja la madarasa mawili makubwa, majengo mawili ya mabweni (Wasichana na Wavulana), Bwalo la chakula na Jiko, Majengo Matatu ya vyoo (Wasichana Wavulana na Watumishi), nyumba mbili za watumishi, jengo la umeme, Jengo la bohari na kibanda cha mlinzi. Kwa wastani hatua ya ujenzi hadi sasa imefikia asilimia 96.

Mwanja alisema mradi wa ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2022 na kuwezesha kutoa nafasi ya kufanya ukamilishaji wa taratibu zingine zenye kuwezesha utoaji wa mafunzo katika chuo.

Alisema chuo kitakapokamilika, kitaendesha mafunzo ya kozi za muda mrefu katika fani za Uhazili na Kompyuta (Secretarial and Computer Application),Ushonaji (Design Sewing and Cloth Technology), Uashi (Masonry and Bricklaying),Umeme wa Majumbani (Electrical Installation),Ufundi Magari (Motor Vehicle Mechanics) na Uchomeleaji Vyuma (Welding and Metal Fabrication). 

Alisema chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 240 wa kozi ndefu na uwezo wa kuchukua wanafunzi 144 wa bweni (wasichana 64 na wavulana 80).

Mwanja aliongeza pia chuo hicho kitatoa mafunzo mafunzo ya muda mfupi (Short Courses) kwa mwezi mmoja hadi miezi sita kwa wanafunzi wapatao 250 hadi 900 kwa mwaka kutegemeana na mahitaji ya jamii na shughuli za kiuchumi za eneo hilo.




No comments:

Post a Comment