Mkuu wa Wilaya ya
Bahi mkoani Dodoma, Mhe. Godwin Gondwe, ametembelea na kukagua maendeleo ya
mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Bahi.
Akizungumza kwenye
ziara hiyo tarehe 15 Februari, 2023, Mhe. Gondwe amesema uwepo wa chuo hicho
utaleta chachu ya mabadiliko ya kiuchumi wilayani hapo kwa kuwa wananchi
watapata ujuzi utakaoongeza thamani katika shughuli zao na kuongeza mapato.
“Tunaamini kabisa
ujuzi utakaotolewa hapa utawasaidia wana Bahi kuongeza uzalishaji katika
shughuli za kilimo, ufugaji na nyingine na hivyo kuleta tija zaidi,”amesema
Mhe. Gondwe ameitaka
VETA kuandaa programu za mafunzo kwa kuzingatia zaidi shughuli za kiuchumi za wananchi
wa Wilaya hiyo ambazo ni ufugaji, kilimo na madini.
Aidha, Mhe Gondwe
ameitaka VETA kutoa kipaumbele kwenye michezo kwa kutenga maeneo ya wanafunzi
kufanya michezo mbalimbali ili kukuza umoja, mshikamano na vipaji wa vijana.
Akitoa taarifa ya utekelezaji
wa mradi huo, Mkuu wa Chuo cha VETA Dodoma Stanslaus Ntibara amesema ujenzi wa
chuo hicho umefikia asilimia 90.
Chuo cha VETA cha
Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa vyuo vipya 25 vya Wilaya nchini ambapo chuo
hicho kinajengwa na kusimamiwa na chuo cha VETA Dodoma kwa kutumia nguvu za
ndani (Force Account).
Ndugu Ntibara ametaja
kozi zitakazotolewa katika chuo hicho kwa awamu ya kwanza kuwa ni Uhazili na
Kompyuta,Ushonaji, Uashi,Ufundi Umeme,Ufundi Magari na Uchomeleaji Vyuma.
Chuo hicho kitakuwa
na uwezo wa kudahili wanafunzi 300 kwa kozi za muda mrefu na 400 kwa kozi za
muda mfupi ambapo nafasi za bweni ni kwa wanafunzi 144.
No comments:
Post a Comment