Aainisha mikakati kuboresha utoaji mafunzo kwenye vyuo vya VETA
Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Prosper Mgaya amefanya
ziara katika Ofisi za VETA Kanda ya Kati na Chuo cha VETA Dodoma ambapo
ametembelea karakana kujionea shughuli za mafunzo na kufanya mazungumzo na
Menejimenti ya Kanda na Chuo.
Akizungumza wakati wa
ziara hiyo leo tarehe 13 Novemba, 2023, Dkt. Mgaya ameainisha mikakati mbalimbali ya kuboresha
utoaji mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi na
kuwawezesha kuendesha shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza ubunifu kwenye kuandaa kozi za muda mfupi zinazojibu mahitaji halisi ya jamii, kuboresha vifaa vya utoaji mafunzo vinavyokidhi ukuaji wa teknolojia na kuhakikisha ubiasharishaji wa vifaa vya kiubunifu vinavyozalishwa kwenye vyuo vya VETA.
“Ni lazima tuongeze ubunifu katika kuandaa
kozi za muda mfupi kujibu changamoto zinazowakabili wananchi kwenye shughuli
zao za kiuchumi…tunafanya vizuri sana kwenye eneo la ubunifu lakini changamoto
ni namna ya kuhakikisha ubunifu huo unaingia sokoni hivyo tunahitaji kuweka
nguvu katika suala hili,”amesema
Dkt. Mgaya ameeleza pia umuhimu wa kupata ithibati za kimataifa kwenye mafunzo yanayotolewa ili kuwezesha wahitimu wa VETA kutambulika kwenye soko la ajira kimataifa na kusisitiza nia yake ya kuwezesha walimu kupata mafunzo na ujuzi ndani na nje ya nchi.
Aidha, Dkt Mgaya
ameeleza kuridhishwa na maandalizi yanayofanywa na Kanda ya Kati kwa ajili
kuanza kutoa mafunzo kwenye vyuo vipya vya ufundi stadi vya Wilaya
yanayotarajia kuanza kutolewa mwezi Januari, 2024 na kumuagiza Mkurugenzi wa
Kanda hiyo kushirikisha viongozi wa Wilaya husika katika maandalizi ya kozi
zitakazotolewa kwenye vyuo hivyo.
Ameelekeza chuo cha
VETA Dodoma kuandaa kozi za aina mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya jamii na
kuzitangaza ili wananchi wazifahamu na kujitokeza kujiunga na kozi hizo ili
waweze kujipatia ujuzi wa kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Dkt Mgaya amesema
mikakati hiyo itachangia kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwapatia watanzania ujuzi
utakaokuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwamba VETA inategemewa kufanikisha
malengo hayo.
Awali, Mkurugenzi wa
VETA Kanda ya Kati, Ndg. John Mwanja
aliwasilisha taarifa ya kanda hiyo inayohusisha mikoa ya Dodoma, Singida
na Manyara ambapo amesema Kanda yake imejipanga vyema katika kuhakikisha vyuo
vilivyopo kwenye kanda yake vinatoa mafunzo bora na kufikia wananchi wengi
zaidi.
Mkuu wa Chuo cha VETA
Dodoma, Ndg.Stanslaus Ntibara, amesema hadi sasa, chuo chake kina jumla ya
wanafunzi 4350 ambapo 650 ni wa kozi za muda mrefu na 3700 ni wa kozi za muda
mfupi ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kutoka mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment