Ujumbe kutoka Korea ya Kusini ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) Tanzania, Bi. Jieun Seory umetembelea VETA ikiwa ni mwendelezo wa ziara yao ya kujifunza shughuli za utoaji mafunzo ya ufundi na ufundi stadi nchini.
Kupitia ziara hiyo
leo tarehe 14 Novemba, 2023, Ujumbe huo umetembelea Ofisi za VETA Makao Makuu
na kupata taarifa ya Mamlaka pamoja na kutembelea chuo cha VETA Dodoma kujionea
namna mafunzo yanavyotolewa pamoja na miundombinu inayotumika chuoni hapo.
Mkurugenzi wa Elimu
ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Dkt. Noel Mbonde amesema Serikali ya Korea Kusini ina mpango wa kujenga chuo
cha ufundi mkoani Morogoro chenye hadhi ya Kimataifa kitakachotoa ujuzi kupitia
programu mbalimbali za kipaumbele katika kukuza uchumi.
“Ujumbe huu umekuja mahsusi kujionea hali
halisi ya utoaji wa mafunzo kwenye vyuo vya ufundi hapa nchini na kupata maoni
yetu juu ya kile tunachohitaji kiwepo kwenye chuo wanachotarajia
kukijenga,”amesema
Dkt. Mbonde amesema
ujumbe huo wa KOICA utaendelea na ziara kwenye vyuo mbalimbali vya ufundi na
mafunzo ya ufundi stadi pamoja na vyuo vya Maendeleo ya wananchi na hatimaye
kujadiliana na Wizara ya Elimu na kukubaliana juu ya ujenzi wa chuo hicho.
No comments:
Post a Comment