Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Prosper Mgaya, amevitaka vyuo vya VETA nchini kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha utoaji wa mafunzo na kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Dkt Mgaya ameyasema hayo tarehe 17 Novemba, 2023
alipofanya ziara katika Ofisi za VETA Kanda ya Dar es Salaam na Chuo cha VETA
Dar es Salaam, kujionea shughuli za mafunzo na kuzungumza na wafanyakazi.
Amesema VETA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika ya Kimataifa na Viwanda kutoa mafunzo na hivyo kuwezesha VETA kuwafikia watanzania wengi zaidi wanaohitaji ujuzi.
“Tumeshuhudia namna utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa ushirikiano na wadau ulivyoweza kunufaisha jamii na sisi wenyewe ndani ya Taasisi yetu… tuendelee kushirikiana kwa karibu na wadau kutoa mafunzo, “amesema
Dkt Mgaya amewaasa wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia ubora ili kuzalisha wahitimu mahiri na kuzidisha jitihada kwenye shughuli za uzalishaji kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani.
Dkt Mgaya pia amesisitiza nia yake ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya VETA yanapata ithibati za kimataifa na kuwezesha ubunifu unaofanyika VETA kubiasharishwa na kuingia kwenye matumizi.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es
Salaam, Ndg. Angelus Ngonyani, amesema Kanda yake imeendelea kubuni programu
mbalimbali za mafunzo kwa lengo la kuimarisha shughuli za kiuchumi hasa za
uzalishaji viwandani, utalii, usafirishaji pamoja na biashara.
Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, Mhandisi Joseph Mwanda, amesema chuo hicho kimeendelea kuwa na ushirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi hali iliyochangia pia kuwezesha upatikanaji wa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Amesema kwa sasa wanafunzi wanaoendelea na mafunzo
kwa kozi za muda mrefu ni 1516 na 3962 wa kozi za muda mfupi kwenye fani 33
zinazotolewa chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment