Wajumbe nane kutoka
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) wametembelea vyuo vya VETA
Moshi na Arusha tarehe 17 Novemba, 2023 ikiwa ni sehemu ya ziara yao katika
vyuo vya VETA, yenye lengo la kujifunza na kujionea jinsi Mafunzo ya Ufundi Stadi
yanavyotolewa nchini.
Ziara hiyo ya siku
mbili, imefanywa na wajumbe hao katika Karakana zaidi ya 10 za vyuo hivyo,
zikiwemo karakana ya Uundaji na Uchongaji Vipuri; karakana ya Ufundi wa Zana za
Kilimo; Karakana ya Uungaji na Uchomeleaji vyuma; Ufundi Bomba; Ufundi Magari;
Ushonaji, Ubunifu wa Mavazi na Teknolojia ya Nguo; Umeme wa Magari; Ukerezaji
Vyuma; Umeme wa Majumbani na karakana ya Elektroniki.
Akizungumza kwa niaba
ya wajumbe hao, Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini, Bi.Jieun Seory amesema,
huo ni mwendelezo wa ziara yao ya kukusanya taarifa zitakazowasaidia katika wa
Ujenzi wa chuo cha ufundi hapa nchini.
"Pamoja na
kupata taarifa mbalimbali za mafunzo na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya
nchi zetu, ziara hii imekuwa sehemu ya kuendelea kujifunza zaidi mbinu
zinazotumika kutoa mafunzo pamoja na kufahamu uhusiano uliopo kati ya sekta ya
utoaji Elimu na Mafunzo na Sekta ya viwanda, ambapo utatupa mwongozo katika
uanzishwaji wa chuo kitakachotoa mafunzo
ya Ufundi kuanzia ngazi za Shahada," amefafanua.
Akiwashukuru kwa ujio
wao katika vyuo vya VETA Moshi na Arusha, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya
Kaskazini, Bi.Monica Mbelle, amewataka wajumbe hao kuendelea kutembelea vyuo
vya VETA ili kufahamu zaidi kuhusu mafunzo yatolewayo na vyuo hivyo nchini na
kubaini maeneo ya ushirikiano.
"Tuna Kanda tisa
zenye vyuo vinavyotoa mafunzo tofauti tofauti nchi mzima, na kwa kuwa ziara hii
imewafanya kuwa sehemu ya familia ya VETA ni vyema sasa mkapanga kutembelea
vituo vingine kupata uelewa wa kina kuhusu Mafunzo yatolewayo na vyuo
hivyo," ameongeza.
Naye Mkurugenzi
Msaidizi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Dkt. Erick Mgaya, amesema, Wizara iko tayari
kushirikiana na KOICA ili kuhakikisha wanafikia lengo la Utoaji mafunzo ya
Ufundi Stadi nchini, hasa ikizingatiwa kwamba sasa ndio msisitizo wa Serikali
ya Awamu ya Sita.
Ziara ya wajumbe hao ilitembelea pia kiwanda cha kuzalisha na kusambaza genereta za Umeme, TANELEC kilichopo eneo la Themi, jijini Arusha ambacho kwa mujibu wa ripoti ya Meneja Uendeshaji wa kiwanda hicho, Ndg. Edrick Mwenda zaidi ya asilimia 60 ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ni wahitimu wa vyuo vya VETA nchini katika fani za Ukerezaji vyuma, Uundaji na Uungaji vyuma na Umeme wa majumbani na viwandani..
No comments:
Post a Comment