Asisitiza ubunifu matumizi ya TEHAMA kutatua changamoto za jamii na kuongeza uzalishaji
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Prosper Mgaya ametembelea Chuo cha TEHAMA cha VETA
Kipawa kujionea shughuli za utoaji
mafunzo na kuzungumza na wafanyakazi wa chuo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo tarehe 16
Novemba, 2023, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mgaya ameagiza Menejimenti na
wafanyakazi wa chuo hicho kuongeza ubunifu katika utoaji mafunzo ya TEHAMA na kuhakikisha
TEHAMA inatumika kwa ufanisi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Amesema chuo hicho maalum kwa ajili ya mafunzo ya
TEHAMA kinategemewa kuzalisha wahitimu mahiri wenye uwezo wa kutumia ujuzi wao
kurahisisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali na kutatua changamoto
zinazoikabili jamii.
“Msisitizo wangu kwenu ni kuhakikisha mnatoa
mafunzo bora, mnafanya ubunifu utakaoweza kutatua changamoto zinazoikabili
jamii yetu na kutoa huduma za kitaalamu kwa jamii na kuongeza mapato ya ndani
ambayo yatasaidia kupunguza utegemezi wa ruzuku toka serikalini katika
kuendesha shughuli za VETA,”amesema
Dkt Mgaya amesema chuo hicho kina fursa kubwa ya
kufanya uzalishaji kupitia utoaji wa huduma mbalimbali za TEHAMA kwa jamii
inayowazunguka na kuwataka kufanya ubunifu na kutumia vyema fursa hizo ili
kujiongezea kipato.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina mategemeo makubwa sana na VETA katika
kuwawezesha wananchi kujipatia ujuzi na kuwataka wafanyakazi kutimiza wajibu
wao kikamilifu ili kufanikisha azma hiyo.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Ndugu
Angelus Ngonyani amemshukuru Dkt. Mgaya kwa kutembelea chuo hicho na kuahidi
kusimamia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa ili kuboresha utoaji mafunzo katika
chuo hicho.
Akisoma taarifa ya chuo, Mkuu wa Chuo cha VETA
Kipawa, Mhandisi Dickson Mkasanga amesema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi
144 wanaoendelea na masomo kwa kozi za muda mrefu katika fani za TEHAMA,
Elektroniki, Umeme wa Majumbani na Umeme wa Viwandani.
Amesema katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi
mwezi Novemba, 2023 chuo hicho kimetoa mafunzo mbalimbali ya muda mfupi kwa wanafunzi 1,890.
Mhandisi Mkasanga amesema chuo hicho kimejipanga
vyema kutoa mafunzo kwenye fani ya mekatroniki ili kuendana na kasi ya ukuaji
na uendeshaji wa viwanda na kwamba kwa sasa chuo kina vifaa vya kisasa kwa
ajili ya kufundishia fani hiyo.
No comments:
Post a Comment