CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Saturday, 16 December 2023

WAHITIMU 1,279 WA UFUNDI STADI WATUNUKIWA VYETI CHUO CHA VETA DODOMA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof Joyce Ndalichako, amewatunuku vyeti wahitimu 1,279 wa mafunzo ya ufundi stadi katika mahafali ya 40 ya chuo cha VETA Dodoma na uhitimishaji wa mafunzo chini ya mradi wa Ujuzi na Ajira kwa Maendeleo (E4D). 

                                                                                   

Kati ya wahitimu hao, 210 ni wa mafunzo ya muda mrefu katika fani 12, 150 mafunzo ya muda mfupi katika fani za udereva na ususi na urembo pamoja na 919 katika fani za Uungaji vyuma viwandani, Ufundi bomba majumbani na ufundi bomba viwandani kupitia Mradi wa E4D. Wahitimu tisa wa E4D wamepatiwa mitaji mbegu kuwawezesha kujiajiri, hivyo kufanya jumla ya vijana waliopatiwa mtaji mbegu kupitia mradi huo kufikia 171.

Akizungumza katika mahafali hayo, tarehe 15 Desemba, 2023, Prof.Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali inayolenga kutoa na kuendeleza ujuzi kwa wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kujipatia ajira.

“Serikali inataka kuona wananchi wengi, hasa vijana wanapata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ambayo yanawapa ujuzi ambao ni msingi muhimu katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii,”amesema 

Prof Ndalichako amewasihi wadau wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Serikali katika kuwezesha utoaji ujuzi na kukuza ajira kwa wananchi na kuitaka VETA kuhamasisha ushirikiano na waajiri ili kutoa mafunzo yanayolingana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Franklin Rwezimula, amesema Serikali inaendelea kuweka miundombinu ya kuwezesha wananchi kujipatia ujuzi bila kikwazo na kwamba ujenzi wa vyuo vya VETA kila Wilaya unalenga kuwaongezea wananchi fursa hiyo.

 

Dkt. Rwezimula ameiagiza VETA kuandaa programu zinazolenga kuongeza thamani kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na wananchi na kutumia vyema vyuo vya Wilaya kuwafikia wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya, amesema VETA imeanza mchakato wa kuwezesha utoaji wa ithibati za kimataifa kwenye mafunzo yanayotolewa ili kuwezesha wahitimu wa VETA kutambulika kwenye soko la ajira kimataifa.

Amesema VETA imejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanajipatia ujuzi na kuongeza tija katika shughuli zao bila kujali kiwango cha elimu walichonacho.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA), Ndg. Manshik Shin amesema Serikali ya Korea inaamini katika kuwapatia ujuzi vijana, hasa kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kuahidi ushirikiano zaidi na Serikali ya Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uongozi na Maendeleo ya Ujasiriamali (IMED), Dkt. Donath Olomi, amesema kupitia mradi wa E4D, vijana walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na kushiriki shindano la mtaji mbegu ambapo jumla ya miradi 67 yenye vijana 171 ilishinda mitaji mbegu ya vitendea kazi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.

Amesema washindi hao pia watapata huduma ya uatamizi wa biashara kwa muda wa kati ya miezi mitatu hadi mitano ambapo watapatiwa huduma za ushauri wa biashara na mafunzo ya uendeshaji wa biashara ili waweze kusimamia imara biashara zao na kuzifanya kuwa endelevu.

Mradi wa E4D ulioanza kutekelezwa mwezi Mei, 2022, ulilenga kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 4000 nchini, katika fani za Ufundi Bomba wa majumbani, Ufundi Bomba viwandani, Ufundi wa Uchomeleaji vyuma viwandani na Ufundi wa Mekatroniki katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Lindi, Manyara na Kipawa kwa lengo la kukuza ajira kwa vijana.

Jumla ya vijana 4,295 wamepata mafunzo na vifaa vya kufundishia vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 vimenunuliwa kupitia mradi huo.





No comments:

Post a Comment