Dirisha la usajili wa ubunifu kwa ajili ya Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) limefunguliwa rasmi, tarehe 9 Aprili 2024.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa
Adolf Mkenda ametangaza kufunguliwa kwa dirisha hilo alipokuwa akizindua Maadhimisho ya Kitaifa ya
Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, kwenye ukumbi wa Wizara, DANIDA, Jijini
Dodoma.
“Dirisha la usajili wa Mashindano ya Kitaifa ya
Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, yaani MAKISATU, limefunguliwa rasmi leo tarehe
9 april 2024 na litafungwa tarehe 8 Mei
2024,” amesema.
Amesema MAKISATU yanahusisha ngazi mbalimbali,
zikiwemo vyuo vya elimu ya juu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya
ufundi na mafunzo ya ufundi na ufundi stadi, shule za msingi, shule za
sekondari na wabunifu kutoka mfumo usio rasmi.
“Mtanzania yoyote mwenye ubunifu wake anakaribishwa kushiriki kwani utakaposhiriki unaongeza fursa ya wewe kusaidiwa na Serikali ili uweze kuendeleza ubunifu wako na kuweza kuuingiza katika soko na katika mpango wa biashara,” amesema.
Amesema, washindi 10 kwenye kila kundi watashiriki
katika fainali zitakazofanyika kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu,
Ujuzi na Ubunifu, jijini Tanga, tarehe 25 hadi 31 Mei, 2024.
Sambamba na MAKISATU, Prof. Mkenda amesema kuwa maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka huu yatahusisha pia Mashindano ya Ujuzi (Skills Competition) yatakayofanyika kwa wanafunzi katika ngazi ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
“Hii ni nyanja mpya, haikuwepo, washindi watano wa
kila fani watashiriki katika maadhimisho ya wiki ya elimu kitaifa na washindi
wa juu watatangazwa na watapewa zawadi mbalimbali katika kilele cha maadhimisho
hayo na wataweza kushiriki katika mashindano ya ujuzi ya kidunia.”
Amesema, Madhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2024 yatahusisha maonyesho ya bidhaa, ubunifu na teknolojia mbalimbali, mashindano ya kitaifa ya sayansi teknolojia na ubunifu yaani (MAKSATU),mashindano ya ujuzi kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi na ufundi stadi nchini, ,mikutano na midahalo kuhusu elimu ujuzi sayansi teknolojia, ubunifu na mafunzo kwa wabunifu.
Amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa na
washiriki kutoka taasisi za umma na binafsi zipatazo 339 na yatatanguliwa na
matukio mbalimbali ambayo yatafanyika katika ngazi za mikoa na halmashauri,
ikiwemo maonesho ya ubunifu na teknolojia, mikutano na midahalo chini ya
uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na wadau wengine.
No comments:
Post a Comment