CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday 5 April 2024

WATUMISHI CHUO CHA VETA NAMTUMBO WATOA MSAADA WA SARE ZA SHULE KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM

 Katika hali ya kuonesha kujali jamii inayowazunguka, watumishi wa Chuo cha VETA Namtumbo wametoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya Msingi na Ufundi Namtumbo iliyopo wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma. Msaada huo wa sare za shule zikiwepo sketi, suruali, kaptula na mashati umetolewa kwa jumla ya wanafunzi 56 wenye mahitaji maalum, wakiwepo wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa chuo cha VETA Namtumbo, wakati wa hafla ya kukabidhi misaada hiyo, tarehe 28 Machi 2024, Mwalimu wa fani ya Uashi kutoka chuo hicho, Salim Dendea, amesema wamefanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa  kufanya jambo ili kuwawezesha wanafunzi hao kupata elimu katika mazingira rafiki.

 “Sisi kama VETA tumeona kwamba watoto wetu hawa wana uhitaji tunaopaswa kuujali sisi wote kwa kuwawezesha kwa kile ambacho kwa kuanzia kinaweza kuwasaidia,” amesisitiza.

Aidha Dendea amewataka wadau na taasisi nyingine za serikali na binafsi, kuiunga mkono shule hiyo, ili kuwasaidia wanafunzi hao hasa wenye mahitaji maalum kila mara wanapoona inawezekana. 

Akisoma risala kwa niaba ya uongozi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi na Ufundi Namtumbo, Mwalimu Bibiana Adam Boyanza, Msimamizi na Mkuu wa Kitengo cha Watoto wenye Mahitaji Maalum amewataka wadau wengine kuendelea kuwaunga mkono, huku akikishukuru chuo cha VETA Namtumbo kwa msaada walioutoa na kuwataka kuendelea kuwasaidia kwa kuwa bado wana mahitaji mengine kama upungufu wa madawati,viwanja vya michezo na visima vya maji ya uhakika. 

“ni rai yangu kuwaita wadau mbalimbali kama walivyofanya VETA kuja kutuunga mkono, na kwa kuwa VETA mnahusika na kutoa mafunzo ya ufundi mnaweza kutusaidia zaidi, na kama mnavyoona kitendo hiki kimeonesha kwamba walemavu sio kwamba hawawezi bali wanaweza wakiwezeshwa,” amesema.

Naye Noel Hassan Kinonono, mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo ameishukuru VETA Namtumbo kwa kuwapa sare hizo na kutoa wito kwa Serikali kuwasaidia kutatua kero mbalimbali zinazowakabili ikiwepo ya upungufu wa walimu wa Ufundi katika shule yao.


No comments:

Post a Comment