Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kampuni ya International Facilities Services Tanzania (IFS) zimesaini hati ya ushirikiano (MoU) kuimarisha utoaji mafunzo ya huduma za hoteli na ukarimu, mahsusi kwa ajili ya kuhudumia sekta madini, mafuta na gesi nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yameingiwa, tarehe 19 Septemba 2024, katika ukumbi wa VETA Makao Makuu, jijini Dodoma, na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Bi. Natasha Main, Afisa Mwandamizi wa Kampuni ya IFS na kushuhudiwa na Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM).
Mkurugenzi Mkuu wa
VETA, CPA. Anthony Kasore, ameyataja yatakayohusika na makubaliano hayo kuwa ni pamoja na kufanya
mapitio ya mitaala inayohusiana na hoteli na ukarimu iweze kukidhi viwango vya
kupata ithibati ya kimataifa na kuwezesha walimu kutoka VETA kupata mafunzo
yatakayoendana na mitaala hiyo mipya ili kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi
bora yenye hadhi ya kimataifa.
CPA. Kasore amesema kuwa, kupitia makubaliano hayo vijana watakaohitimu katika vyuo vya VETA watapata ujuzi utakaowawezesha kupata ajira popote katika sekta ya ukarimu, madini, mafuta na gesi.
“Naiomba kampuni ya IFS kuwezesha hoteli zetu
za VETA katika maeneo mbalimbali ikiwemo zikiwemo za Arusha, Mtwara, Dodoma na
Morogoro ili ziweze kutoa huduma bora katika kiwango cha kimataifa,” CPA Kasore
ameongeza.
Mwakilishi wa IFS nchini Tanzania, Bi. Marie Ragwe makubaliano hayo yatawezesha vijana watakaohitimu kupitia vyuo vya VETA kupata ajira ndani na nje ya nchi kwa kuwa watakuwa na sifa zenye ubora wa kimataifa katika sekta ya hoteli, ukarimu, madini, mafuta na gesi.
Mtendaji Mkuu wa Bodi
ya Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka amepongeza makubaliano hayo kwa kuwa
yataongeza ujuzi bora kwa vijana wa Kitanzania kwa kupata mafunzo yenye hadhi
ya kimataifa na kuweza kuajiriwa ndani na nje ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment