Dar es Salaam, Desemba
2, 2024 – Imeelezwa kuwa Serikali ina jukumu muhimu katika kuimarisha
ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, elimu, na viwanda ili kujenga mfumo
thabiti wa ubunifu.
Hayo yameelezwa na Kanali (mstaafu) Joseph Simbakalia wakati akizungumza katika Mkutano na Maonyesho ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu (STICE), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JICC), Dar es Salaam, ubiasharishaji leo, Desemba 2, 2024.
Simbakalia, afisa mstaafu
wa jeshi na kiongozi wa Serikali, alikuwa
akitoa mada kuu juu ya "Kurekebisha Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu
(STI) ili Kuimarisha Ushirikiano wa Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi",
ambapo amesema kuwa mafanikio ya ushirikiano huo yanahitaji juhudi za makusudi
kutoka kwa Serikali ili kuimarisha uendelezaji na ubiasharishaji ubunifu.
Ameweka wazi umuhimu wa kutunga sera, sheria, na Serikali kutoa maelekezo yenye lengo la kufikia mafanikio katika uendelezaji teknolojia na ubunifu.
Aliitaja Korea Kusini kama mfano bora, ambapo maagizo ya serikali yalifanikisha uunganishaji wa sekta binafsi (viwanda) na taasisi za utafiti na elimu ili kubadilisha mawazo bunifu kuwa bidhaa zinazoweza kuingia sokoni.
"Nafikiri tuna changamoto kubwa katika ubunifu wa sera kuliko ubunifu wa bidhaa," ameongeza.
Katika mjadala, CPA
Anthony Kasore, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
(VETA), naye ameunga mkono maoni ya Simbakalia.
Amesisitiza umuhimu wa sera thabiti kuimarisha uhusiano na kuboresha mawasiliano ya kimkakati na ushirikiano kati ya wadau, ikiwa ni pamoja na viwanda na jamii, ili kubaini na kushughulikia mahitaji ya ujuzi na jamii.
Kasore ametoa mfano
kuhusu ubunifu mwingi ndani ya VETA,
akitaja kuwa walimu, wanafunzi, na wahitimu wake ambao wameunda teknolojia
mbalimbali za kiubunifu, lakini nyingi hazijabiasharishwa kutokana na ukosefu wa mtaji na ushiriki wa kutosha wa
sekta binafsi yenye utashi wa kuzichukua na kuzalisha kwa wingi.
"Ingawa wanafunzi wetu wanaonyesha ubunifu na ufanisi wa ajabu, tunahitaji mifumo thabiti ya msaada ili kubadilisha mawazo yao kuwa mafanikio ya kibiashara," amesema.
Mkutano na Maonesho ya
Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE) yanawaunganisha watafiti, wabunifu,
sekta binafsi, na watunga sera, na yanaendelea kutumikia kama jukwaa la
kubadilishana mawazo na kuchunguza mikakati ya kuimarisha mfumo wa ubunifu wa
kitaifa.
Washiriki walitoa wito wa hatua za kivitendo kuziba mapengo kati ya elimu, utafiti, na viwanda, kuhakikisha kwamba sayansi, teknolojia, na ubunifu vinachukua nafasi kuu katika mabadiliko ya kiuchumi ya Tanzania.
STICE 2024, inayofanyika kuanzia Desemba 2 hadi 4, inalenga kukuza mazungumzo na ushirikiano ili kushughulikia changamoto muhimu na kutumia fursa katika mfumo wa ubunifu.
No comments:
Post a Comment