Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeibuka mshindi wa kwanza katika Mashindano ya Mama Lishe yaliyofanyika katika uwanja wa Zakhiem uliopo Mbagala, wilaya ya Temeke, jijini Dar es salaam, tarehe 4 Desemba, 2024.
VETA imewakilishwa na
mshiriki Neema Andrew Mwang'ombe, mwanafunzi
wa fani ya Uandaaji Chakula, kutoka chuo cha VETA cha mkoa wa Dar es
salaam, alieibuka mshindi wa kwanza dhidi ya washiriki wengine zaidi ya 250
waliojiandikisha na kuingia katika kinyang' anyiro cha mashindano hayo yanaratibiwa na East Africa TV na Radio.
Neema amesema haikuwa
rahisi kuibuka mshidi wa kwanza katika Mashindano hayo kwa kuwa ushindani
ulikuwa mkubwa hasa ukizingatia kwamba yamehusisha Mama Lishe kutoka mikoa yote
ya Tanzania Bara na visiwani.
"Mashindano haya
yalikuwa na ushindani wa hali ya juu na kila Mama mshiriki alitamani kuwa
mshindi, lakini juhudi, kumtanguliza Mungu na ujuzi nilioupata kupitia Mafunzo ya ufundi stadi kutoka katika chuo
cha VETA yamenifanya kuwa mshindi," ameongeza.
Mwalimu Euphrasia
Mushi wa fani ya Uandaaji Chakula, kutoka chuo cha VETA cha mkoa wa Dar es salaam ameongeza kuwa
kumekuwa na juhudi za hali na mali
zinazofanywa na VETA katika kuhakikisha kwamba inazalisha jamii ya watu wenye
Ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Nae Anna Sombida,
mratibu wa Mashindano hayo kutoka kituo cha runinga na redio cha EATV amesema mashindano hayo yanalenga
kumwongezea Mama lishe thamani na uwezo katika kutenda majukumu yake ya kila
siku hasa kwenye eneo la chakula na lishe.
Mashindano hayo
yanaingia msimu wa tano toka kuanzishwa kwake na kwa mwaka huu yamefanyika
katika Wilaya 5 za mkoa wa Dar es salaam, ambapo yalianza rasmi tarehe 30 Oktoba, 2024 katika Uwanja wa Mwinjuma
wilaya ya Kinondoni na baadae kuendelea
Mnada wa ndizi, Kabibo wilaya ya Ubungo, Uwanja wa Kampala relini- Gongo
la mboto wilaya ya Ilala, Uwanja wa Zhakiem Mbagala wilaya ya Temeke na
yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 11 Desemba, 2024 katika wilaya ya Kigamboni.
Mshindi wa kwanza
katika Mashindano hayo amezawadiwa fedha taslimu shilingi 600,000/- kutoka
Airtel, Jokufu moja kutoka Kampuni la Jedan Home Store, Kiwanja chenye ukubwa
wa mita za mraba 500 kutoka Kampuni la Mwendapole, akaunti ya Imbeju na benki
ya CRDB yenye amana ya kuanzia na kupata Mafunzo ya mwezi mmoja katika eneo la
Mapishi kwenye chuo cha Taifa cha Utalii (NCT).
Vilevile, mshindi
atapewa nafasi ya kutangaziwa biashara yake kupitia EATV na Radio.
Mshindi wa pili
amepewa Kiwanja cha mita za mraba 500, Brenda moja, kusoma mafunzo ya mapishi
kwa muda wa mwezi mmoja katika chuo cha Teknolojia na Utawala
cha Kilimanjaro
(KITM), Account ya Imbeju yenye amana ya kuanzia, pesa taslimu shilingi
400,000/ kutoka Airtel na mshindi wa tatu amepata shilingi 300,000/- kutoka
Airtel, Jiko la sahani mbili na kiwashio chake kutoka Jaden Home Store.
No comments:
Post a Comment