CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday, 24 April 2026

Naibu Waziri Wanu ahimiza ushirikiano VETA na viwanda kuimarisha ujuzi na ajira kwa vijana

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuendelea kuimarisha mikakati ya kushirikiana na viwanda ili kuibua fursa zaidi za ajira na ujuzi kwa vijana nchini.

Mhe. Hafidh ametoa wito huo tarehe 23 Aprili, 2026 wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya ufundi wa aluminium na ufungaji wa vioo kwa wakufunzi na mafundi wa fani ya useremala jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limeambatana na uzinduzi wa mtaala mpya wa mafunzo hayo yanayoendeshwa na kampuni ya Emirates Aluminium Profile kwa kushirikiana na VETA yenye lengo la kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inaendana na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha rasilimali watu kwa kuzingatia kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia duniani.

“Ushirikiano kati ya vyuo vya VETA, sekta ya uzalishaji, waajiri na viwanda ni muhimu ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira,”amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mafunzo kwa wakufunzi ni hatua muhimu itakayosaidia kuboresha ubora wa ufundishaji na kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira.

Amesema awamu ya kwanza imehusisha wakufunzi 18 wa fani ya useremala watakaopatiwa ujuzi wa vitendo unaohitajika viwandani.

CPA Kasore amebainisha kuwa wakufunzi hao watajengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo makadirio ya vifaa na gharama, uundaji wa miundo ya aluminium, ufungaji wa vioo, utengenezaji wa samani za chuma na ufungaji wa dari.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Emirates Aluminium Profile, Deogratius Marandu, amesema mafunzo hayo yataongeza thamani kwa mafundi na kuwapa utambuzi unaohitajika katika soko.

Ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.




No comments:

Post a Comment