CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday, 5 May 2026

VETA na Airtel Tanzania wasaini makubaliano ya kuimrisha mafunzo ya ufundi stadi kidigitali kwa vijana nchini


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA imesaini makubaliano na kampuni ya mtandao wa simu wa AitelTanzania kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya ufundi satdi kwa njia za kidigiatali (VSOMO APP), programu ambayo itawawezesha vijana kujifunza stadi mbalimbali popote walipo kwa kutumia simu za mkononi au vishikwambi.

Makubaliano hayo yamesaini leo, tarehe 5 Mei, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Airtel Tanzania, Bw. Charles Kamoto kwenye ofisi za Airtel Tanzania, Kinondoni jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa hati ya makubaliano iliyosainiwa, makubaliano hayo yanalenga kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa njia za kidigitali, kwani kupitia VSOMO APP mtu atapata mafunzo ya nadharia (theory) moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi au kishikwambi, hivyo hatahitaji kuwa darasani muda wote.

Hati hiyo imefafanua kuwa baada ya kumaliza masomo ya nadharia kwenye simu, mwanafunzi atachagua chuo chochote cha VETA kilicho ili kukamilisha mafunzo ya vitendo.

Aidha kupitia VSOMO APP mwanafuzi ataweza kujifunza masomo  ya ufundi kwa lugha na Kiswahili au Kingereza, jambo linalomwezesha mwanafunzi kuelewa kwa urahisi.

Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amesema VSOMO APP ni jukwaa kubwa linalowaweza wananchi kupata mafunzo kwa njia ya kidigitali kupitia teknolojia ya simu,kompyuta na vishikwambi.

“kwa upande wetu sisi kama VETA tumekuwa tukiutumia mfumo huu,kulingana na jukumu tulilonalo lakutoa mafunzo  mfumo huu unatusaidia kuwafikia watanzania popote walipo kwa urahisi” amebainisha Kasore.

CPA Kasore ameongeza kuwa jukwaa la VSOMO APP pia limeunganishwa na mfumo wa Fundi Connect, unaowawezesha wahitimu wa VETA kusajili ujuzi wao na kuunganishwa moja kwa moja na wateja, hivyo kuimarisha uhusiano kati ya mafunzo na ajira pamoja na kusaidia ujasiriamali wa vijana.

Sambamba na hilo Kasore amesema ushirikiano huo unaunga mkono ajenda ya maendeleo ya Taifa chini ya Dira ya Maendeleo 2030, na kuimarisha juhudi za Serikali za kuongeza ajira kwa vijana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

¬“Tunaishukuru sana Airtel Tanzania kwa msaada wao endelevu, hasa katika kutoa huduma ya intaneti na kuwezesha upatikanaji mpana wa VSOMO. Ushirikiano huu umetuwezesha kuwafikia vijana wengi zaidi kuliko hapo awali. Lakini pia tunaishukuru Serikali ya kwa kuendelea kuwekeza katika  Elimu na mafunzo ya ya ufundi stadi,” amesema Kasore

Amebainisha kuwa kupitia VSOMO, VETA imelenga kuwafikia wanafunzi wapya 400 kila mwezi, kama sehemu ya kuendelea kupanua mafunzo ya ujuzi kidigitali na kuimarisha ajira kwa vijana nchini.

“Kupitia VSOMO, tunapanua wigo ili vijana wengi zaidi wapate ujuzi wa vitendo kwa ajili ya ajira na kujiajiri popote walipo,” amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Airtel katika kuendeleza mageuzi jumuishi ya kidigitali na kupanua upatikanaji wa elimu ujuzi kwa Watanzania.

“Airtel VSOMO ni jukwaa rasmi la taifa la mafunzo ya ufundi stadi mtandaoni chini ya VETA. Linawawezesha Watanzania kupata ujuzi wa vitendo wakati wowote na mahali popote kupitia vifaa vyao vya kidigitali,” amesema Kamoto.

Kamoto amesisitiza kuwa mchango wa Airtel hauishii kwenye mawasiliano pekee, bali unajumuisha uwekezaji mpana katika ujumuishaji wa kidigitali, elimu na uwezeshaji wa vijana.

_“Sisi Airtel hatujihusishi tu na kutoa huduma ya mtandao. Tunahamasisha kikamilifu matumizi ya Airtel VSOMO, tunatoa huduma ya bila gharama ya data, na kuhakikisha gharama si kikwazo kwa Watanzania kujifunza na kujiendeleza,”_ameongeza


Naye Beatrice Singano, Mkurugenzi wa mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania amesema VSOMO inasiadia vijana wengi kujifunza kupitia mtandao huku wakiendelea na shughuli zao nyinge za uzalishaji.

_“tuliwauliza vijana wengi wakasema kozi za VETA zina manufaa makubwa kwao, lakini hawana muda wa kwenda kukaa darasani muda mrefu, hivyo kwa kupitia VSOMO vijana watatumia muda mchache kusoma kupiti simu zao, huku wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji bila kuathirika”_amesema.

Takwimu za Airtel zinaonesha kuwa Airtel VSOMO imepakuliwa mara 59,000, ambapo takribani asilimia 60 ya matumizi yamefanyika kupitia huduma ya bure ya data ya Airtel. Jumla ya watumiaji 27,194 wamejisajili kwenye jukwaa hilo, huku wanafunzi 9,539 wakijiunga na programu mbalimbali za ufundi stadi.

Kati ya hao, wanafunzi 6,723 tayari wamehitimu mafunzo yao, jambo linaloonesha ongezeko la matumizi na mafanikio katika elimu ya ufundi stadi ya kidigitali.

No comments:

Post a Comment