CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday, 7 August 2026

PROGRAMU YA ESPJ II KUFADHILI VIJANA 14,000 WAISHIO MAZINGIRA MAGUMU KUJIFUNZA UFUNDI STADI

 

Vijana 14,000 wanaoishi katika mazingira magumu nchini watanufaika na elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia mpango maalum wa ufadhili wa Programu ya Pili ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi zenye Tija (ESPJ II), hatua inayotarajiwa kuongeza ujuzi, ajira na fursa za kujitegemea kwa kundi hilo.

Mpango huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya VETA na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) chini ya Programu yaESPJ II), inayofadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa majadiliano ya utekelezaji wa mpango huo, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema taasisi hiyo ipo tayari kutekeleza jukumu kupitiia mtandao mpana wa vyuo zaidi ya 80 inavyomiliki kote nchini.

Alisema uwezo huo utaiwezesha VETA kuwafikia wanufaika wote 14,000 ndani ya kipindi cha miaka miwili, huku ikitekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuingia katika soko la ajira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, CPA Mwanahamis Chambega, amesema TEA inaendelea kuendesha Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) chini ya programu ya ESPJ II, huku ushirikiano na VETA ukiwa nguzo muhimu ya kuhakikisha walengwa wanafikiwa kwa wakati.

Naye Mratibu wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), Masozi Nyirenda, amesema programu hiyo itadumu kwa miaka sita na wanufaika watapatiwa mafunzo ya muda usiozidi mwaka mmoja katika sekta 10 za kipaumbele, zikiwemo kilimo na biashara ya kilimo, ujenzi, nishati, TEHAMA, utalii na ukarimu, madini, mifugo na uvuvi, afya, usafirishaji na uchukuzi pamoja na uzalishaji viwandani.

Amesema ushirikiano na VETA utarahisisha utekelezaji wa mpango huo kutokana na uwepo wa miundombinu na uzoefu wa taasisi hiyo katika kutoa mafunzo ya ufundi nchini.

Majadiliano hayo yalihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kuharakisha maandalizi ya mkataba wa ushirikiano utakaoweka msingi wa kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mpango huo.

1 comment:

  1. When selecting an exterior material, durability and low maintenance are important considerations. Fiberglass siding can be a practical choice for projects that need a reliable and attractive finish.

    ReplyDelete