Mwenyekiti wa Bodi ya
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Profesa Sifuni Mchome,
amezitaka taasisi za Serikali kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza bunifu
zinazozalishwa nchini ili zifikie hatua ya kuzalishwa kibiashara, kuongeza ajira
na kuchochea ukuaji wa uchumi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050.
Profesa Mchome ametoa wito huo, tarehe 5 Agosti 2026, alipotembelea banda la VETA katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya taasisi za Serikali, amesema ameridhishwa na kiwango cha ubunifu kinachoendelea kufanywa nchini na kusisitiza kuwa ushirikiano wa taasisi hizo ni nguzo muhimu ya kuhakikisha bunifu hizo zinakuzwa na kuwanufaisha wananchi pamoja na uchumi wa taifa.
"Nimefurahi
kupata nafasi ya kutembelea mabanda mbalimbali na kujionea bunifu zinazofanywa
na taasisi za serikali. Nimeona bunifu za hali ya juu. Haya yanaonyesha kuwa
Tanzania ina uwezo mkubwa wa ubunifu," amesema.
Akizungumzia
kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka huu isemayo, "Tambua Soko, Ongeza
Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," Prof. Mchome amesema
inalenga kuwahamasisha wadau wa uzalishaji kutambua fursa za masoko, kuongeza
thamani ya bidhaa na kuimarisha mnyororo wa thamani kupitia ushirikiano.



No comments:
Post a Comment