![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEipT3wwxydbbo56WbKR5aRcc-kKfYPJvSdLRCy7Ww9r0KmB_-qilrtSc1aXmXv_nS46wu3hNkf643zltysFh54GFnd3nSdjpy0Y9IDXLiBlPGl0s4-53QL71DnoBRHTCMqs6B-eRNpOXrMk/s400/veta+sabasaba.jpg)
Wakati
maonesho ya Sabasaba yakiwa na kaulimbiu isemayo, “Ukuzaji wa Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda,” VETA ilikoleza kwa
ujumbe, “Viwanda Vinahitaji Ujuzi, Ujuzi
Unapatikana VETA”
Takwimu
za mahudhurio ya watu katika banda la VETA zimeonesha kuwa takribani watu
59,101 wakiwemo wageni mashuhuri 19 walitembelea banda la VETA katika kipindi
chote cha maonesho kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, 2017, idadi ambayo
imeongezeka zaidi ya mara dufu ukilinganisha na mwaka jana (2016) ambapo idadi
ya wahudhuriaji ilikuwa yapata 26,000.
Wengi
wa watu waliotembelea banda la VETA walionesha kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na
huduma zake, ambapo 58,788 (96%) walisema maonesho ya huduma za VETA ni mazuri
sana, 2207 (3.7) mazuri na 324 (0.54%) wastani.
Licha
ya kupata watu wengi wakitembelea banda lake, VETA ilifanikiwa kuibuka mshindi
katika kundi la Uendelezajii Ujuzi na Mafunzo na kuwa mshindi wa pili wa jumla
wa maonesho ambayo yalishirikisha taasisi, makampuni na mashirika 2520 kutoka
nchi 31.
Akizungumzia
maonesho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dr. Bwire Ndazi alisema kumekuwa
na mwamko mkubwa wa wananchi kutembelea banda la VETA kutokana na kutambua
fursa mbalimbali za ujuzi pamoja na ubunifu ambao umekuwa ukioneshwa na VETA
kila mwaka.
“idadi
ya watu imekuwa ikiongezeka kila mwaka kwa sababu kila mara wanaona vitu vipya,
vitu vinavutia, vinahamasisha vijana na watu wengine kuhusu ujuzi na ubunifu
mbalimbali,” alisema.
Aliongeza
kuwa, katika maonesho hayo, VETA ililenga pia kuonesha jinsi ambavyo imejipanga
kuisaidia serikali kuandaa nguvukazi yenye ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya
viwanda.
Miongoni
mwa wageni mashuhuri waliotembelea banda la VETA ni pamoja na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles John Mwijage ambaye pamoja na mambo
mengine, aliipongeza VETA kwa ujumbe mzuri unaohamasisha watu kujifunza ujuzi
ili washiriki kikamilifu katika uanzishaji na uendelezaji viwanda.
Naye Rais wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Ali Hassan Mwinyi alivutiwa na maendeleo ya VETA katika kusimamia na kuendeleza ufundi stadi nchini, akisema kuwa kumekuwa na ubunifu na umahiri mkubwa unaooneshwa na wanafunzi na walimu wa ufundi stadi na akaishauri VETA kuzidi kujitangaza zaidi na kutangaza ubunifu mbalimbali ili umma uzidi kutambua umuhimu wa ufundi stadi.
No comments:
Post a Comment