Jumla ya vijana 102 waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam wamepatiwa vifaa vya kufanyia kazi ili kuwawezesha kujiajiri.
Wahitimu waliokabidhiwa
vitendea kazi chini ya mradi huo wa YEE ni wale ambao wameunda vikundi vyao na
kuvisajili rasmi.
Akikabidhi vifaa hivyo
kwenye hafla fupi iliyofanyika katika chuo cha VETA Dar es Salaam tarehe 18
Julai, 2017 Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke, Hashimu Komba alipongeza hatua
hiyo na kuwataka vijana kutumia vifaa hivyo walivyovipata kuboresha shughuli
zao za kiufundi kulingana na fani walizosoma, hivyo kujiingizia kipato.
Aliwataka watendaji wa
Wilaya na Kata kuweka utaratibu wa kufuatilia kwa karibu vikundi hivyo na
kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuwatafutia suluhisho.
“Fursa hii mliyoipata
leo ni ya kipekee na mna wajibu wa kutendea haki mafunzo mliyoyapata na mkakae
na kupanga matumizi sahihi ya vifaa hivi,” alisema
Komba aliahidi kuwa wilaya
yake itahakikisha inawaandalia vijana hao mazingira rafiki ya kuwawezesha
kufanya shughuli zao kwa kuwapatia mikopo nafuu na kuwapatia zabuni mbalimbali
zinazoendana na fani zao na kuzitaka ofisi za kata kufanya hivyo ili kuunga
mkono jitihada za vijana hao.
Meneja Mradi wa Plan International
Adolph Jeremia alisema kuwa vifaa hivyo vyenye thamani ya Shilingi 12,613,742
vimetolewa kwa vikundi vya vijana waliohitimu
fani za Umeme Majumbani, Ushonaji, Udereva, Ufundi magari,Uchomeleaji na
Uungaji vyuma na mapishi na mapambo.
Alisema vijana 155
waliohitimu kati ya 257 hawajapata fursa ya kupewa vifaa kutokana na kutojiunga
katika vikundi, hivyo akawashauri pia
kujiunga na kusajili vikundi vyao ili waweze kunufaika na mpango wa kupatiwa
vifaa.
Mmoja wa wanufaika wa mradi
huo Anna Nkembo aliyesoma fani ya ushonaji amesema mafunzo kupitia mradi huo
yamebadilisha maisha yake kwani baada tu ya kuhitimu amejiajiri na anashona
nyumbani kwake na kujipatia kipato cha kujikimu.
Alisema upatikanaji wa vifaa
hivyo kupitia kikundi chao cha wahitimu nane utawasaidia kufanya kazi nyingi na
punde wataanza kutafuta zabuni za kushona nguo nyingi zaidi hasa sare za
wanafunzi.
Mradi wa YEE
unatekelezwa kwa ushirkiano kati ya VETA, Plan International, VSO, CORDET,
UHIKI na CCBRT katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara .
No comments:
Post a Comment